Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akizungumza na timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii wakati timu hiyo ilipofika mkoani hapo kwa lengo la kukisanya maoni kutoka kwa wadau wa Maendeleo ya Waanwake na Jinsia katika kuboresha Sera yao.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango sehemu ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sophina Mjangu akitoa maneno ya awali kabla ya ufunguzi wa kikao kazi cha wadau wa maendeleo ya Wanawake na Jinsia waliokutana na Wizara kujadili na kutoa maoni katika kuboresha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia mkoani Singida.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Hanifa Selengu akifafanua jambo katika kikao kazi cha wadau wa maendeleo ya Wanawake na Jinsia waliokutana na Wizara kujadili na kutoa maoni katika kuboresha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia mkoani Singida.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Singida ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Bw. Stanslaus Choaji akifungua kikao kazi cha wadau wa maendeleo ya Wanawake na Jinsia waliokutana na Wizara kujadili na kutoa maoni katika kuboresha Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia mkoani Singida.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
*************************************
Na Mwandishi Wetu Singida
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeamua kufanya tathimini ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya mwaka 200 na Mkakati wa utekelezaji wa mwaka 2005 ili tathimini hiyo isaidie kufanya mapitio ya Sera itakayozingatia makubaliano ya mikataba mbalimbali, Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Mpango wa pili wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano na maoni ya wadau.
Haya yameelezwa leo mkoani Singida na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sera na Mipango sehemu ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Sophina Mjangu wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichowakutanisha wadau wa maendeleo ya wanawake na Jinsia kutoka mikoa ya Singida, Dodoma na Tabora na Wizara.
Bi. Sophina amesema kuwa madhumuni ya Sera iliyopo yalikuwa ni kutoa mwelekeo ambao ungehakikisha kuwa mipango, Mikakati na shughuli mbalimbali za uongozi na maendeleo katika kila Sekta na Taasisi inazingatia usawa wa kijinsia.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kupitia Sera hiyo ni kuifanya iendane na wakati na iwezi kubeba mabadiliko yaliyojitokeza katika miaka kumi na tisa tangu kandaliwa kwake mwaka 2000 ikiwemo changamoto katika utekelezaji wa Sera hii ikiwemo mapungufu yake na nini kifanyike ili kuiboresha Sera ili kueandana na wakati husika.
“Hii itatokana na maoni ya wadau tutakayoyapata inawezekana ikawa mpya au tukabadilisha na jina la Sera ili tunawasikiliza wadau ili nadhani yote yanawezekana” alisema Bi. Sophina
Akifungua kikao kazi hicho kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Bw. Stanslaus Choaji amesema kuwa Kikao hicho kinatarajia kufikia malengo ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake katika kufikia maendeleo jumuishi hususan katika Sekta ya Afya, Elimu, Kilimo na Masuala ya kifedha, uwezeshaji wa wanawake katika nafasi za uongozi na siasa, mazingira na Uzazi na Afya ya Mtoto na kukusanya Taarifa na Takwimu zitakazowezesha kuandaa Rasimu ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia.
Ameongeza kuwa kikao kazi hicho kitawezesha kukusanya maoni yatayowezesha kuwa na Sera Shirikishi inayozingatia masuala yote muhimu na kupata uelewa wa pamoja kuhusu wajibu wa Serikali na wadau katika uwepo wa Sera ya maendeleo ya Wanawake na Jinsia .
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii mkoa wa Singida Bw. Jonathan Simiti amesema kuwa Sera hiyo inatakiwa kufanyiwa maboresho ingawa kuna juhudi za Serikali katika kuondokana na Unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi kwa hivyo Sera isaidie wanawake kuwezeshwa katika kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Nimesikia kwenye redio kuwa wanawake sasa wanaendesha magari makubwa kama malori na mabasi ya abiria masuala ya kijinsia yamekuwa kwa kiasi kikubwa nchini ukilinganisha na wakati uliopita” alisema Bw. Simiti.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Singida Bi. Shukranui Mbago amesema kuwa Sera iliyopo ni nzuri na inatekelezeka ingawa kuna mambo muhimu yanatakiwa kuingizwa ikiwemo umiliki wa mali na kutoa maamuzi kwa watoto wa kike na wanawake katika ngazi ya Kata.
“Unakuta Mwanamke au mtoto wa kike anatafuta pesa lakini kwa asilimia kubwa zinamilikiwa na wanaume na watoto wa kiume tunahitaji Sera isisitize umiliki wa mali na utoaji wa maamuzi hasa katika Kaya kwa mtoto wa kike na mwanamke” alisema Bi. Shukrani.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika machakato wa kukusanya maoni kwa wadau kutoka Kanda saba za Tanzania Bara ili kuwezesha maboresho ya Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000.