Madarasa mawili yaliyo kwisha kujengwa Shule ya Msingi Isingiwe.
Na Dotto Mwaibale, Singida
MBUNGE wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe amekagua Kituo cha Afya cha Kata ya Mitundu na ujenzi wa Shule ya Msingi Isingiwe na ujenzi wa vyoo Shule ya Sekondari ya Mitundu iliyopo wilayani Itigi mkoani Singida na kuzungumza na mganga mfawidhi wa kituo hicho Sister Sarah Tidias ili kujua changamoto zilizopo.
Akizungumzia changamoto zilizopo katika kituo hicho Sister Tidias alisema wanaukosefu wa maji ambapo hutumia kutoka kwenye visima viwili ambayo huyavuta kwa kutumia mikono na kuwa hakina umeme mbadala baada ya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kukatika.
“Umeme wa Tanesco ukikatika tunalazimika kutumia tochi kumsaidia mjamzito wakati wa kujifungua” alisema Sister Tidias.
Tidias alitaja changamoto nyingine kuwa kituo hicho kina watumishi wachache, hakina gari la kubebea wagonjwa kwa ajili ya kuwapeleka Hospitali ya Rufaa.
Alitaja changamoto nyingine kuwa wanauhaba wa majengo kama jengo la upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya wanawake na wanaume, jengo la kufulia, kuhifadhia maiti, nyumba za watumishi na uzio kuzunguka kituo hicho.
Alitaja huduma zinazotolewa katika kituo hicho kuwa nikutibu wagonjwa wa nje ambao kwa mwezi hufikia watu 800 na zaidi, wajawazito ambao kwa mwezi uliopita walikuwa 95 na kliniki ya watoto kwa mwezi wanahudumia watoto 120.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa shule ya Isingiwe yenye madarasa mawili yaliyokamilika Afisa Mtendaji wa Kata ya Mitundu, Raphael Ackley alisema kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kuwapunguzia safari ndefu ya wanafunzi wa eneo hilo kwenda kusoma shule ya Msingi Makale na kupunguza idadi ya watoto wanaosoma Shule ya Msingi ya Mitundu ambayo imeelemewa na wingi wa watoto.
Mbunge Mattembe baada ya kupokea maelezo hayo alisema atayawasilisha kwa wahusika kuona namna ya kuyashughulikia ambapo pia aliweza kutoa mashuka na sabuni ambazo aliwapatia wagonjwa na watumishi wa kituo hicho.