Nabu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akizungumza mbele ya Wajumbe kutoka mahakamani wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga, Gerson Mdemu (wakwanza kushoto waliokaa), wakati wa Kikao, lengo ikiwa ni kuona jinsi taasisi zinazohusika na hukumu kushirikiana kwa pamoja katika kutenda haki na kuepusha ucheleweshwaji wa kesi.Kikao hicho kimefanyika mkoani Simiyu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga, Gerson Mdemu akizungumza na Nabu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni(katikati),wakati wa kikao cha kujadili mambo mbalimbali yanayohusu utolewaji hukumu na ucheleweshwaji wa kesi mbalimbali.Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka. Kikao hicho kimefanyika mkoani Simiyu.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
*****************************
Na Mwandishi Wetu-Simiyu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amezitaka taasisi mbalimbali zinazoshughulika na kutoa hukumu na maamuzi kufanya kazi kwa pamoja ili kuwaokoa wananchi wanyonge waliopo katika magereza mbalimbali nchini.
Ameyasema hayo Mkoani Simiyu wakati wa Kikao cha pamoja kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wajumbe kutoka mahakamani wakiongozwa na Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga, Gerson Mdemu na Wajumbe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka.
Akizungumza katika kikao hicho Naibu Waziri Masauni alisema kama mihimili muhimu katika maamuzi ya watanzania wenzetu waliopo magerezani tunatakiwa kukutana mara kwa mara ili kuweza kuona ni vipi tunaweza kuwatoa wale wasio na sababu za msingi za kubakia magerezani
“Wote tulipokea maagizo ya Mheshimiwa Rais baada ya kutembelea gereza Butimba ambapo alitoa agizo vyombo husika vikutane ili kuweza kusikiliza kero za mahabusu wanaokaa muda mrefu bila kesi zao kushughulikiwa na hilo linaenda sambamba na kila chombo husika kutenda haki na kuzingatia maadili katika kazi zake,mfano kumekua na malalamiko baadhi ya mahakimu kupokea rushwa au askari wetu kubambikia watu kesi,si jambo nzuri kumuweka mtu asiye na hatia gerezani,” alisema Masauni.
Akizungumza katika kikao hicho Jaji Mfawidhi Kanda ya Shinyanga,Gerson Mdemu, alisema wao kama mahakama wamejipanga kuhakikisha hukumu zinaenda na sasa wanauleta utaratibu katika mabaraza ya mikoa ili madai mengine yaanze kushughulikiwa katika ngazi za chini ili kupunguza mzigo na mrundikano wa kesi
“Nipo na wajumbe hawa kutoka mahakamani tukitembelea mikoa yote ya Kanda ya Ziwa, lengo kubwa ni kuona ni jinsi gani shughuli za mahakama zinaenda bila kuleta matatizo yoyote kwa wananchi ikiwepo uharakishaji wa kesi mbalimbali, zingine zikianzia ngazi ya chini na kumaliziwa katika eneo husika,” alisema Jaji Mdemu
Naibu Waziri Masauni yuko ziara katika mkoa wa Simiyu akikagua shughuli mbalimbali za taasisi zilizopo chini ya wizara yake ambapo alipata nafasi ya kupitia Vituo mbalimbali vya polisi mkoani hapo na kuongea na mahabusu.