Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo (wa tatu kulia), akikata utepe wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 150 kwa Shule ya Msingi, Mkunguni, Hananasif pamoja na Sekondari ya Hananasif. Kulia kwake ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo (kushoto), akipokea sehemu ya msaada wa madawati 150 yaliyotolewa na Benki ya NMB kutoka kwa Meneja wa benki hiyo Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Changolo (kulia), akipokea sehemu ya msaada wa mabati 180 kwa ajili ya Shule ya Msingi Turiani kutoka kwa Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki. Benki ya NMB ilitoa madawati 150 kwa shule ya Msingi Hananasif, Mkunguni pamoja na Shule ya Sekondari Hananasif.
Mwanafunzi wa Darasa la V Shule ya Msingi Mkunguni, Jane Shija, akimshukuru Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam baada ya kukabidhi msaada wa madawati 150.
Baadhi ya wanafunzi wakiwa wamekaa katika madawati mapya waliyokabidhiwa na Uongozi wa Benki ya NMB.
***********************************
Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Daniel Chongolo, ameimwagia sifa Benki ya NMB kwa jinsi inavyojitolea katika miradi ya maendeleo nchini wakati alipokuwa akipokewa msaada wa madawati na mabati kwa shule nne za Kinondoni, uliotolewa na Benki hiyo leo jijini Dar es Salaaam.
NMB kupitia Meneja, Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd walikabidhi msaada wa mabati 180 kwa ajili ya Shule ya Msingi Turiani, Madawati 150 kwa shule za msingi, Hananasif, Mkunguni pamoja na shule ya sekondari Hananasif.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Hananasif Sekondari Chongolo alisema, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Benki hiyo kwani imekuwa ikigusa sekta mahsusi za Elimu, Afya na Miundombinu nchini kote.
“Kwa dhati napenda kutoa shukrani zangu kwa Benki ya NMB kwa jinsi ambavyo imekuwa mstari wa mbele kutoa misaada na kuunga mkono juhudi za Serikari ya Awamu ya tano katika kutatua chanagamoto zinazowakabili watanzania.
“Msaada huu wa mabati na madawati kwa shule hizi unaenda kuongeza chachu ya vijana wetu kupata Elimu katika mazingira rafiki kwa kipindi cha miaka mitano.” amesema Chongolo na kuongeza.
“Binafsi napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa NMB kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakiunga juhudi za Serekali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa kutoa misaada katika maeneo mbali mbali ya nchi.
Chongolo alisema shule hizo zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa miundombinu ya kujifunzia kwa wanafunzi na kuahidi kuwa Serikali inayafanyia kazi mapungufu yaliyopo, kwa kushirikiana na sekta binafsi kuzitatua.
Kwa upande wa Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam Badru Idd, amesema misaada hiyo ni sehemu ya misaada ambayo NMB imepanga kuitoa kwa mwaka ambapo kila mwaka hutenga Bilion 1, huku mwaka huu wameshatoa misaada zaidi ya Milioni 800 ikiwemo hiyo waliyoitoa kwenye shule hizo.
“Kama NMB ni utaratibu wetu wa kurudisha kwa jamii katika kile tunachokipata kila mwaka, jamii ndio tunayoihudumia na ndio wateja wetu. Katika Bilioni 1 tunayoitenga kila mwaka hadi sasa tumeshatoa zaidi ya Milioni 800.
“Leo tuko hapa kwa ajili ya kutoa msaada wa Mabati 180 kwa shule ya Tuliani, Madawati 50 kwa Shule ya Msingi ya Hananasif, Madawati 50 kwa Shule ya Sekondari ya Hananasifu na 50 mengine kwa Shule ya Msingi ya Mkunguni.” alisema Idd.