Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akizungumza na wananchi wa
Kata ya Tura Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Tabora.
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja
na Mbunge wa Igalula Mhe. Musa Ntimizi, Mkuu wa Wilaya ya Uyui Bi. Gift Msuya
pamoja na wananchi.
**********************************
Serikali imejipanga kutumia zaidi ya Shilingi milioni 300 kutatua tatizo la maji katika Kata ya Tura iliyopo Halmashauri ya Uyui jimbo la Igalula mkoani Tabora.
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) amesema wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Tura katika Halmashauri ya Uyui mkoani Tabora.
Waziri Mbarawa amesema mwezi huu Novemba, 2019 serikali itapeleka Shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa mradi wa maji ili kuondoa tatizo kubwa la maji linalowakabili wananchi wa Kata ya Tura.
Amesema fedha hizo zitahusisha ujenzi wa pampu ya kusukuma maji kutoka kwenye bwawa hadi katika tanki, ambalo litakalojengwa mita 12 kwenda juu, kununua bomba kubwa lenye kipenyo cha milimita 160 kwa urefu wa kilomita 5 kutoka kwenye bwawa mpaka kwenye tanki na ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji lita laki mbili pamoja na mtandao wa kusambaza maji kwa wananchi.
Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa (Mb) ametaka utekelezaji wa kazi hiyo kufanyika kwa kutumia Watalaam wa Wizara ya Maji, na siyo Mkandarasi.
Wengine watakaohusika ni pamoja na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa mazingira Tabora (TUWASA), RUWASA na kuwashirikisha wananchi kwa kuchimba mitaro ya kulaza mabomba.
Hata hivyo, Waziri Mbarawa amewataka Wahandisi wa Wizara ya Maji kuongeza kasi zaidi ya utekelezaji ili kuleta tija katika kuwapatia wananchi majisafi na salama.
Katika kikao hicho, Waziri Mbarawa alifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Uyui Bi. Gift Msuya, Mbunge wa Jimbo la Igalula Mhe. Musa Ntimizi, Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA Mhandisi Joel Rugemalila na viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.