**********************************
Na Mwandishi Wetu
Serikali ya Awamu ya Tano imeuwezesha mkoa wa Mbeya kujenga miundombinu ya kisasa katika sekta zinazochangia kuleta ustawi kwa wananchi ikiwemo afya.
Akizungumza katika kipindi cha ‘TUNATEKELEZA’ Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe.Albert Chalamila amesema kuwa mkoa huo umepiga hatua kubwa katika kuleta mageuzi kupitia miundombinu iliyojengwa katika sekta za afya, elimu, maji, uchukuzi na kilimo.
“Serikali imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika mkoa wetu na ziko katika hatua za mwisho kukamilika ili ziweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali kuboresha sekta hiyo” Alisisitiza Chalamila.
Akifafanua, mhe. Chalamila amesema kuwa mkoa huo umefakiwa katika ujenzi wa Vituo vya Afya hali inayoboresha huduma zinazotolewa katika sekta hiyo katika Halmashauri za Wilaya mkoani huo.
Sehemu ya Halmashauri za Wilaya zilizonufaika na ujenzi wa Hospitali za Wilaya ni; Rungwe,Busokelo na Kyela,pamoja na upanuzi na ujenzi wa Vituo vya Afya ili
kutimiza lengo la Serikali kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote.
Katika sekta ya Elimu Mhe. Chalamila amesema kuwa Shilingi Bilioni 18 zimetolewa katika kuboresha sekta hiyo hivyo kukuza kiwango cha elimu na ubora kutokana na uwekezaji huo uliofanywa na Serikali.
“Tumejipanga katika kukuza sekta ya viwanda na tumetenga eneo maalum la
uwekezaji wa viwanda vidogovidogo na tayari baadhi ya wajasiriamali wa mkoa huo wamepata fursa ya kwenda nchini China kujifunza namna ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vya usindikaji mbogamboga na matunda,” Aliongeza Chalamila.
Akieleza zaidi, amesema kuwa mkoa huo umeweka mkazo katika kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta mbalimbali ili kuboresha hali ya maisha.
Aidha, Katika Halmashuri ya Wilaya ya Busokelo, Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya hiyo utakaogharimu shilingi Bilioni 5.3 ili kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Wilaya ya Rungwe Bi
Rehema Peter amesema kuwa utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi Bilioni 5 utawanufaisha wananchi zaidi ya elfu ishirini.
“Kukamilika kwa mradi huu wa maji kutaongeza wananchi wanaofikiwa na huduma ya maji kutoka asilimia 65 hapo awali hadi kufikia asilimia 80 hali itakayochochea kukua kwa shughuli za kiuchumi na ustawi wa wananchi.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Bw. James Kasusura amesema kuwa wamefanikiwa kuvuka lengo la makusanyo katika robo ya kwanza ya mwaka 2019/2020 kwa kukusanya shilingi Bilioni 3.1 sawa na zaidi ya asilimia 26 ya lengo walilojiwekea.
Tumeweza kukarabati nyumba 25 za walimu katika Jiji letu na pia tumejenga kituo cha afya Nzowe kwa shilingi milioni 700 zilizotolewa na Serikali.
Kipindi cha TUNATEKELEZA kinaratibiwa na Idara ya Habari MAELEZO na kurushwa na Shrika la Utangazaji Tanzania, Awamu hii ikiwashirikisha Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara.