Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani nje ya ukumbi wa mikutano katika halmashauri ya mji kibaha akizungumzia kuhusina na msimamo wake pamoja na madiwani juuu ya kuyataifisha maeneo ambayo watu wake wamehindwa kuyaendeleza.
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha Leornad Mlowe akifafanua jambo kwa waandishi wa habari hawapo picha kuhusiana na maazimio waliyoyafikia katika kikao cha baraza la madiwani kuhusiana na chanagamoto ya kukithiri kwa mashamba pori na kuyataifisha kwa yale maeneo ambayo hayaendelezwi,
Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya mji Kibaha wakiwa katika kikao cha kujadili mambo mbali mbali ya maendeleo ikiwemo kuweka msimamo juu ya kuyataifisha maeneo yote ambayo yamegeuka kuwa mashamba pori
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya mji Kibaha Jenipher Omolo akielezea jambo kwa waandishi wa habari kuhusina na mikakati ambayo wameiweka katika kukabiliana na changamoto ya kuwepo kwa mashamba pori ambayo yamekuwa ni kero kwa kipindi kirefu.(PICHA NA VICTOR MASANGU)
………………………………………………….
VICTOR MASANGU, KIBAHA
BARAZA la madiwani katika halmashauri ya mji Kibaha mkoani Pwani limeazimia kwa pamoja kuingilia kati sakata la maeneo ambayo yametelekezwa kwa kipindi kirefu bila ya kuendelezwa na kupelekea kuwa mashamba pori hivyo wameamua kuyataifisha yote ndani ya kipindi cha miezi miwili endapo bado yataonekana bado hayajaendelezwa.
Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa halmashauri ya mji Kibaha Leornad Mlowe kwa niaba ya baraza la madiwani ambapo amebainisha kuwa tatizo hilo limekuwa sugu kwa kipindi cha muda mrefu hivyo wamechoshwa na hali ambapo wataandika barua rasmi kwa Waziri mwenye dhamana ili sheria na taratibu ziwewe kuchukua mkondo wake ikiwemo pamoja na kufuta kabisa hati za wamiliki wa maeneo hayo.
“Sisi kama baraza la madiwani la halmashauri ya mji kibaha baada ya kukaa kikao chetu cha kawaida tumeweza kujadili mambo mbali mbali ya maendeleo lakini kubwa zaidi tumeamua na kukubaliana kwa pamoja ni kutaifisha maeneo yote ambayo hayajaendelezwa kwa kipindi kirefu na sisi tumetoa muda wa miezi miwili kwa wahusika kuyaendeleza mtu ambaye atakaidi basi hatua zitachukuliwa kwani hii hali imekuwa ni tatizo na lengo letu ni kuleta maendeleo kwa wananchi,”alisema Mlowe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Kibaha mji Jenipher Omolo alikiri kuwepo kwa baadhi ya watu kutoyaendeleza maeneo yao kwa miaka zaidi ya mitatu kinyume kabisa na sheria na taratibu za ardhi hivyo kusababisha ukosefu mkubwa wa mapato na kuzolotesha kasi ya maendeleo kwa wananchi kutokana na baadhi ya maeneo hayo kuwa mapori makubwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama ambaye ndiye aliwasilisha hoja yake binafsi katika kikao cha baraza la madiwani kuhusiana na kukithiri kwa maeneo mengi kuwa mapori amebainisha kuwa nia ya serikali ya awamu ya tano ni kuwa na Tanzania ya viwanda hivyo watu wote walioyatelekeza maeneo yao yatarudishwa kwa serikali na kubadilishiwa matumizi mengine.
Mshama aliongeza kuwa katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Kibaha kuna changamoto kubwa ya kuwepo kwa maeneo ambayo yamegeuka kuwa mashamba pori kutokana na wahusika kutoyaendeleza kabisa hivyo kwa sasa atahakikisha anashirikiana bega kwa bega na madiwani pamoja na mamlka zinazohusika ili kuweza kuyarudisha maeneo hayo kwa serikali ilinyatumike katika shughuli nyingine za kimaendeleo.
“Kwa kweli ndugu waandishi ili tatizo la kuwepo kwa mashamba pori katika mji wetu wa kibaha limekuwa ni la miaka mingi sana na tayari nilishaambia kuwa maeneo yote ambayo yamechukuliwa ni lazima yaendelezwa na sio kuyaacha kwa miaka mingi bila ya kuyafanyia kitu chohote lakini kuna baadhi ya watu bado wamekuwa ni wagumu na lengo letu kubwa ni kuona mji wetu una kuwa ni sehemu ambayo sio mapori kama ilivyo kwa sasa,”alisema Mshama.
Kumekuwepo na wimbi la baadhi ya maeneo katika Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani kutoendelezwa kwa kipindi cha miaka mingi hivyo kupelekea kugeuka kubwa mashamba pori na mengine kuwa vichaka vikubwa ambavyo vimekuwa ni sehemu ya wahalifu kwenda kujificha pindi wanapofanya matukio mbali mbali ya uporaji.