Mwanasheria Mkuu wa Serikali Profesa Aderladus Kilangi akihitimisha kikao kazi cha siku mbili baina yake na Wakurugenzi wa Sheria na Wakuu wa Vitengo vya Huduma za Sheria kutoka Wizara, Taasisi za Serikali, Mashirika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kikao hicho kimefanyika Jijini Dodoma na kuhimitishwa jana ( Alhamisi).
******************************
Na Mwandishi Maalum,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi
amewaasa Wanasheria wa Serikali katika Utumishi wa Umma
kukubali mabadiliko, kubadilika na kujibadili vinginevyo jamii
itawabadili.
Ameyasema hayo jana ( alhamisi) jijini Dodoma, wakati
akihitimisha kikao kazi cha siku mbili baina yake na
Wakurugenzi wa Sheria na Wakuu wa Vitengo vya huduma za kisheria
kutoka Wizara,Mashirika, Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa pamoja na Taasisi mbalimbali za serikali.
“Tumekutana hapa kwa siku mbili, tumejadiliana mafanikio na
changamoto zinazotukabili katika taaluma yetu, tumebadilishana
mawazo ili sote tuwe na picha ya pamoja, niwashukuru kwa
michango yenu, mawazo yenu na na mapendekezo yenu sura moja na
na lengo letu ni moja tu tunajenga nyumba moja ambayo ni
serikali ambayo mwisho wa siku tuijengee nchi yetu na watu wake
na hii nchi inamatarajio yake, inamatumaini yake na sisi ni
sehemu ya mchakatao huo”.
"Lakini niseme kwa namna moja ama nyingine picha ya
wanasheria katika jamii siyo nzuri sana, tunaweza kuwazungumzia
mawakili wa kujitegemea lakini pia wanasheria wa serikali wamo
katika mkumbo huo " amesema Mwanasheria Mkuu.
Na kwa sababu hiyo akawataka wanasheria hao wa Serikali kwamba
wanalazimika kubadirika."tusipobarilika tutabadirishwa na jamii,
tutabadirishwa na mazingira na hii ni kwa wanasheria wote hata
mawakili wa kujitegemea “Profesa Kilangi akabainisha kwa kusema "mtu wa mtaani anaangalia namna gani haki inatendeka, namna gani mambo
yanayomgusa katika maisha yake yanathaminiwa na kutekelezwa kwa misingi ya haki, haangalii mbwembwe zako au lugha unayoongea
hayo hayamhusu anataka haki itendeke kwa hiyo kubadirika ni
lazima, kujibadilisha ni wajibu na lakini ili ufanye mabadiriko
yatakayokuacha salama lazima ujitengenezee utaratibu unataka
ubadirike vipi na kwa namnma gani na ndiyo sababu ya kukutana
hapa kwa siku mbili”.
Amewaeleza Wanasheria hao katika utumishi wa umma kwamba
serikali na nchi kwa ujumla imo katika mabadiliko makubwa. “Na
sisi ni sehemu ya mchakato huo wa kuijenga nchi na hasa
kushughulikia matatizo ya watu katika eneo hili la sheria”.
Akizungumzia zaidi kuhusu mabadiriko, Profesa kilangi amesema,
mabadiliko huambatana na wasiwasi na taharuki na kwamba hata
miongoni mwa wanasheria hao wa serikali wapo wenye wasiwasi
lakini akawahakikishia kwamba mabadiriko hayo hayalengi katika
kumkomoa mtu bali ni katika kuboresha utekelezaji wa majukumu
yao na kuwajengea mazingira bora zaidi kama Wanasheria wa
Serikali.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho,
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Huduma za Sheria Ofisi ya Rais-
TAMISEMI Bw. Eustard Ngatale amemshukurua Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kwa kuandaa kikao kazi hicho na kuomba Miongozo
mbalimbali iliyowasilishwa kwao ikamilike haraka ili waweze
kuitumia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Rasimu ya Miongozo iliyowasilishwa kwa Wanasheria hao ni
Muongozo wa kutunga sheria ndogo;Muongozo ya upekuzi wa Mikataba
mbalimbali;Muongozo wa majadiliano ya Mikataba yote;Muongozo wa
usimamizi wa utekelezaji wa Mikataba na Muongozo wa utoaji wa
ushauri wa kisheria.
Vile vile katika kikao kazi hiki wanasheria wa Serikali
walisitizwa kuhakikisha kwamba hukumu zinazotolewa na mahakama
baada ya kesi kumalizika zinatekelezwa ili kuepuka matatizo
yanayotokana na kutotekelezwa kwa hukumu hizo.
Bw.Ngatala amesema Kikao kazi hicho baina yao na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali kimewapa matumaini na faraja kubwa kwamba sasa
wanamahali pakuzungumzia mafaniko na changamoto wanazokabiliana
nazo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Vile vile kwa niaba ya washiriki, Bw Ngatala wamekubaliana na
hoja ya kubadilika katika utekelezaji wa majukumi yao na
kwenda kusimamia taaluma yao.
Wanasheria hao wamependekeza vikao kazi hivi kufanyika mara kwa
mara kwa lengo la kuelimishana na kuweka sawa katika
kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao kwa welendi na
tija.