Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akishirikiana na wafugaji kuingiza ng’ombe kwenye josho la Kijiji cha Kikonko wilayani Mlele mkoani Katavi wakati wa uzinduzi wa uogeshaji mifugo awamu ya pili na kutangaza ng’ombe mmoja sasa ataogeshwa kwa sh 50 tu badala ya sh 500 waliokuwa wanatozwa miaka ya nyuma.Picha na Mpiga Picha Wetu
Na Mwandishi Wetu, Katavi
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amezindua kampeni ya kitaifa ya uogeshaji mifugo nchini na kutangaza neema kubwa kwa wafugaji ambapo sasa ng’ombe mmoja ataogeshwa kwa shilingi 50 badala ya sh 500 huku Mbuzi na Kondoo wakiogeshwa kwa sh 10 kila mmoja.
Uamuzi huu wa Serikali utawawezesha kuokoa shilingi bilioni 19 ambazo wafugaji wangezitumia kuogesha mifugo yao lakini ambapo sasa itatumika shilingi bilioni 2.16 tu huku Serikali ikiwapatia wafugaji ruzuku ya asilimia 90 ambapo kama wafugaji wangeendelea na bei hiyo ya miaka ya nyuma wangelazimika kutumia sh bilioni 21.6.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa Kampeni ya uogeshaji mifugo awamu ya pili katika Josho la Kikonko wilayani Mlele na baadae mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Majimoto, Waziri Mpina alisema kupitia mpango huo Serikali itasambaza dawa ya ruzuku lita 12, 546 kwenye majosho yanayofanya kazi 1,733 nchini kote.
Huku Mvua kubwa ikinyesha kwenye mkutano huo, Waziri Mpina alitumia zaidi ya saa moja kuhutubia huku akinyeshewa na mvua na kuwathibishia wananchi kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuleta mageuzi kwa vitendo hasa katika sekta ya mifugo.
Alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM Ibara ya 25 kipengele inaiagiza Serikali kuhakikisha mifugo yote inaogeshwa ili kuweze kuzuia magonjwa yote yanayoenezwa na kupe ambapo asilimia 72 ya vifo vya mifugo vinasababishwa na kupe.
Hivyo uogeshaji huo utawezesha mifugo kujikinga na maradhi na vifo ambapo Serikali itaogesha michonyo milioni 38 kwa Ng’ombe, michonyo milioni 18 ya Mbuzi, michovyo milioni 7 ya Kondoo, na michovyo 2500 ya Punda hivyo utaliwezesha taifa kupata mifugo bora ambayo haina magonjwa.
Waziri Mpina alibainisha kuwa katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja Serikali imekarabati majosho 400 na kwamba majosho yaliyobaki ambayo hayajakarabatiwa ni 639 na kusisitiza kuwa yote yatakarabatiwa ili kuongeza kasi ya uogeshaji mifugo.
Waziri Mpina alisisitiza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya magonjwa ya binadamu yanasababishwa na mazao ya mifugo ikiwemo nyama na maziwa hivyo uamuzi wa Serikali kuogesha mifugo pia umelenga kupambana na magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Hivyo juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono na watendaji wote wa Serikali, wafugaji wote ili kuboresha afya za mifugo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo ikiwemo nyama, maziwa na ngozi sambamba na kuwakinga wananchi na maradhi yanayoweza kuambizwa kutoka kwenye mifugo.
Kufuatia uzinduzi huo, Waziri Mpina ameagiza kila kijiji nchini kiwe na josho kwenye vijiji vyote zaidi ya 12,000 ili kila kijiji kiweze kuogesha mifugo na kusisitiza kuwa Serikali ya Rais Magufuli itakuja na mkakati wa kuhakikisha kila kijiji kinapata josho kama sehemu ya kuboresha afya za mifugo.
Pia ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha majosho yote yamekarabatiwa ndani ya mwezi mmoja na wizara itahakikisha inasambaza dawa kwenye majosho yote mabovu.
Aidha amesisitiza wanaokwenda kuogesha mifugo wafuate sheria za uogeshaji kuhakikisha mifugo inaogeshwa lakini kwa fedha ambayo Serikali imeitangaza ya sh 50 kwa kichwa na ng’ombe na sh 10 kwa kichwa cha mbuzi na zoezi hili litafanyika mfululizo kwa kipindi cha miezi 6 na kumuagiza Mkurugenzi wa huduma za mifugo, Madaktari ya Mifugo wa Mikoa, na Wilaya kuhakikisha zoezi hilo linasimamiwa vizuri kuhakikisha wananchi hawatapeliwi
Pia Waziri Mpina ameweka wazi kuwa Serikali itatangaza bei elekezi ya chanjo ifikapo 15 Novemba mwaka huu na hakuna mtu mwingine atakayekwenda kuwaibia wafugaji tena na kwamba chanjo ya homa ya mapafu ya ng’ombe itauzwa kwa sh 350 tofauti na siku za nyuma ambapo walichanja kwa sh 2000 kwa kichwa cha ng’ombe.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Komredi Juma Homera amemhakikishia Waziri Mpina kuwa Serikali ya mkoa huo inatasimamia maagizo yote na kwamba hakuna mfugaji atakayeonewa au kudhulumiwa na kwamba bei elekezi iliyotangazwa ya sh 50 kwa kichwa ngombe na 10 kwa mbuzi italeta neema kubwa kwa wafugaji.
Pia kuhusu malalamiko ya wafugaji kupigwa faini kubwa kuuawa kwa mifugo yao amemkabidhi nyaraka za malalamiko hayo Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Katavi na kuwakamata watu wote waliotajwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Hezron Nonga amesema zoezi hilo la ugeshaji litafanyika nchi nzima na kuwataka wafugaji kujitokeza kuogesha mifugo yao ili kuikinga na maradhi.