Home Mchanganyiko SERIKALI YAPONGEZA JUWANATA KWA KUANZISHA JUMUIYA YA WASINDIKAJI NAFAKA

SERIKALI YAPONGEZA JUWANATA KWA KUANZISHA JUMUIYA YA WASINDIKAJI NAFAKA

0

Mjumbe wa kamati ya Juwanata Aminiel Maro akisoma rasimu ya Katiba ya umoja huo,wakati wa mkutano maalum kujadili na kupitisha katiba hiyo kwa wajumbe leo jijini Dar es Salaam.

 Mwenyekiti wa muda wa Jumuiya ya Wasindikaji Nafaka ( JUWANATA) Oscar Munisi akiongea wakati wa ufunguzi wa mkutano maalum wa katiba wa jumuiya hiyo jijini Dar es Salaam .Lengo la mkutano huo ni kupitisha katiba itakayoongoza wasindikaji nafaka nchini katika kutafuta suluhisho la masoko ya bidhaa.

Baadhi ya wajumbe wa mkutano maalum wa kupitisha katiba ya kuanzisha Jumuiya yawasindikaji nafaka nchini wakifuatilia mada za mkutano leo jijini Dar es Salaam.

 Mkurugenzi Msaidizi -Masoko ya mazao Wizara ya Kilimo Benito Kavenuka akitoa salamu za wizara wakati wa ufunguzi wa mkutano maalum wa Jumuiya ya Wasindikaji Nafaka nchini.Mkutano huu umefanyika leo Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wasindikaji nafaka toka mikoa yote.

*******************************

Dar es Salaam 30.10.2019

Serikali imeupongeza uongozi wa muda wa Jumuiya ya Wasindikaji Nafaka
Tanzania (JUWANATA) kwa kukamilisha rasimu ya katiba ya umoja wao
Pongezi hizo za serikali zimetolewa leo na Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo
cha Masoko toka Wizara ya Kilimo Benito Kavenuka wakati wa mkutano
maalum wa Juwanata uliofanyika Jijini Dar es Salaam .

Kavenuke amesema kuundwa kwa jumuiya ya wasindikaji mazao ya nafaka
ni utekelezaji wa azimio la mkutano wa wafanyabiashara ya mazao ya
nafaka uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu chini ya Waziri wa Kilimo.

“Serikali inaunga mkono Juwanata kwa kutekeleza kwa haraka azimio la
mkutano wa Waziri wa Kilimo na wafanyabiashara wa nafaka la kuanzisha
jumuiya hii muhimu kwa ustawi wa viwanda vya mazao ya nafaka.”
alisema Kavenuka.

Aliongeza kusema serikali itapenda kuona Viongozi wa jumuiya hii
wanasimamia viwango vya ubora wa bidhaa za nafaka zinazalishwa ili
kuwa na uhakika wa soko na bei nzuri.

Kavenuka amewataka pia kuongeza wigo wa kuwafikia wasindikaji waliopo
mikoani kujiunga na jumuiya hii,ili serikali pamoja na wadau wengine wa
maendeleo iwe rahisi kutoa huduma za kukuza sekta ya usindikaji nafaka
nchini.

Akitoa taarifa ya mkutano huo maalum,Mwenyekiti wa muda wa Juwanata
Oscar Munisi alisema lengo la jumuiya ni kuitikia kwa vitendo kauli mbiu
ya serikali ya kujenga viwanda vya kuongeza thamani mazao ya nafaka .

Munisi aliongeza kusema jumuiya yao inaundwa na wanachama wamiliki
wa viwanda vya kusindika nafaka na mafuta toka mikoa yote ya Tanzania
bara ambapo kazi ya kuandaa katiba ya muda ilishirikisha wadau wote
“Tunataka kuwa na Katiba itakayosaidia kusajili wasindikaji wote nchini
hususan wajasiliamali wadogo ili tuwe na sauti ya pamoja katika kuyafikia
masoko ya bidhaa za nafaka kwa ushirikiano na serikali” alisema Munisi.

Alitaja changamoto ya wajasiliamali wasindikaji kwa sasa nchini kuwa ni
kufikia masoko kama ya Lubumbashi Kongo imekuwa ngumu kwa
kukosekana chombo cha kuwaratibu.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Baraza la Nafaka la Afrika Mashariki
(EAGC) Ikunda Terry amewataka wasindikaji hususan wa mchele
kuongeza ubora ili kufikia soko kubwa la nchi za Uarabuni.

“Tanzania ina fursa ya soko la uhakika la mchele kwani sasa uzalishaji
umefikia tani 2,200,000 wakati matumizi ya ndani kwa mwaka ni kama
tani milioni moja,kwa hiyo tunayo ziada ya zaidi ya tani milioni moja kwa
ajili ya kuuza nje ya nchi” alisisitiza Ikunda.

Kufanyika kwa mkutano huu maalum kunafatia mkutano wa Waziri wa
Kilimo Japhet Hasunga alioitisha hapo tarehe 29 na 30 Agosti mwaka huu
kujadili changamoto za masoko ya mazao ya nafaka nchini.