Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare wakati akikagua Mtambo Mtambo wa Kuchuja Chumvi “Reverse Osmosis” uliogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 2.3 utakaotumika kwa Mradi wa Maji wa Gairo, mkoani Morogoro.
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akitoa maelekezo ya kumaliza kazi ya Mradi wa Maji wa Gairo kwa Wakandarasi wa Kampuni ya Protecno Srl ya Italia wanaosimamia kazi ya ufungaji wa mtambo a pampu za kusukuma maji.
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa akiwa na baadhi ya wageni wa meza kuu katika hafla ya kupokea Mtambo wa Kuchuja Maji ya Chumvi “Reverse Osmosis” kwa ajili Mradi wa Maji wa Gairo, mkoani Morogoro.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), Mhandisi Tamim Katakweba akitambulisha timu ya wataalam itayokuwa ikisimamia uendeshaji wa Mtambo wa Kuchuja Maji ya Chumvi “Reverse Osmosis” kwa ajili Mradi wa Maji wa Gairo, mkoani Morogoro.
Sehemu ya Mtambo wa Kuchuja Maji ya Chumvi (Reverse Osmosis) uliogharimu Sh. bilioni 2.3 utakaotumika kwenye Mradi wa Maji wa Gairo, wilayani Gairo, mkoani Morogoro.
Sehemu ya Mtambo wa Kuchuja Chumvi “Reverse Osmosis” uliogharimu Sh. bilioni 2.3 utakaotumika kwenye Mradi wa Maji wa Gairo, wilayani Gairo, mkoani Morogoro.
……………………
Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa amesisitiza Serikali itachukua hatua zozote zinazostahili ili kumaliza kabisa tatizo la maji kwa wananchi katika maeneo yote yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji ikiwemo Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro.
Kauli hiyo imekuja akiwa katika Wilaya ya Gairo kukagua Mtambo wa Kuchuja Chumvi (Reverse Osmosis) uliogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 2.3 uliowasili kutoka nchini Italia utakotumika kwenye Mradi wa Maji wa Gairo akitimiza ahadi aliyoitoa alipokuwa ziarani mkoani Morogoro miezi michache iliyopita.
Prof. Mbarawa amesema Serikali imetumia gharama kubwa kununua mtambo huo kwa kuwa inawathamini wananchi wake na haitasita kuchukua hatua zozote zinazostahili katika kutimiza azma yake ya kufikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2020.
Pia, amesisitiza pamoja na kufungwa kwa mtambo huo, inafanya utaratibu wa kutafuta chanzo kingine cha maji kitakachoongeza uzalishaji wa maji yatakayotosheleza na kumaliza tatizo la Maji kwa Mji wa Gairo.
Prof. Mbarawa amesema ifikapo mwezi Novemba, 2019 mradi utaanza kutoa huduma kwa wananchi na kumtaka Mkandarasi, Kampuni ya Protecno Srl ya Italia kumaliza kazi ya ufungaji wa mtambo na pampu haraka.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Loata Ole Sanare ameishukuru Wizara ya Maji kwa kuchukua hatua ya kuukamilisha mradi huo ambao umechukua muda mrefu na kutimiza ahadi ya kuleta mashine hiyo itakayoimarisha kiwango cha ubora wa maji, ambayo kwa maeneo ya Gairo yana changamoto kubwa ya chumvi nyingi.
Akisisitiza Serikali imepeleka takribani Shilingi bilioni 16 katika Wilaya ya Gairo kwa dhamira ya kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji na kuishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wa Gairo kwa kusikia kilio chao cha mahitaji ya huduma ya majisafi na salama, hususan kwa Mji wa Gairo unaokua kwa kasi wenye wakazi wapatao 55,000.
Miongoni mwa wakazi wa Gairo wamesema kuwasili kwa mashine hiyo, ambapo baadhi yao walidiriki kudhihaki kuwa ahadi ya Waziri wa Maji ni porojo kwa kuwa wameshaahidiwa ahadi lukuki bila kutimiziwa, wamesema hakika Serikali imedhamiria kutatua kero ya maji katika wilaya yao yenye tatizo kubwa la maji kulinganisha na maeneo mengine Morogoro. Huku wakisema wanasubiri kwa hamu kubwa maji hayo ifikapo mwezi Novemba ili waweze kufurahia matunda ya Serikali yao.
Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Gairo unatekelezwa kwa pamoja na wakandarasi wa Kampuni za Serengeti Ltd na Protecno Srl chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) kwa gharama ya zaidi ya Shilingi bilioni 10, umelenga kuhudumia wananchi wapatao 32,808 na utainua kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 38 kwa sasa mpaka asilimia 80 utakapokamilika.