Miss Tanzania 2019 Sylivia Sebastian (kulia) akisistiza jambo wakati wa uzinduzi
wa taulo za kike (Uhurupads) uliofanyika katika shule ya sekondari Moshono leo jijini
Arusha.
Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico (kushoto) na Miss Tanzania 2019
Sylivia Sebastian (kulia) wakifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa taulo za kike
(Uhurupads) uliofanyika katika shule ya sekondari Moshono leo jijini Arusha.
Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley
(kushoto) akisisitiza kufurahishwa kwake na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya
Tanzania ambapo ni mara ya kwanza kwake kuja nchini. Kulia ni Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe.
Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico (kushoto) na Miss Tanzania 2019
Sylivia Sebastian (kulia) wakiwa katika moja ya matukio wakati wa uzinduzi wa taulo
za kike (Uhurupads) uliofanyika katika shule ya sekondari Moshono leo jijini Arusha.
Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico akisisitiza jambo wakati wa
uzinduzi wa taulo za kike (Uhurupads) uliofanyika katika shule ya sekondari Moshono
leo jijini Arusha.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe
akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa taulo za kike (Uhurupads) uliofanyika katika
shule ya sekondari Moshono leo jijini Arusha.
(Picha na Eleuteri Mangi, WHUSM, Arusha)
*******************************
Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Arusha
Ni heshima kubwa kwa Tanzania kutembelewa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa
Shindano la Miss World Bi Julia Morley pamoja na Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa
Ponce.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe wakati wa uzinduzi wa taulo za kike zinazojulikana kama Uhurupads
uliofanyika leo katika shule ya sekondari Moshono iliyopo jijini Arusha.
“Ujio wao leo hapa Arusha, ni heshima kwa taifa. Katika mataifa yote duniani,
wameichagua Tanzania, hii ni heshima kubwa na wametuletea zawadi ya Uhurupads
ambazo zitawaweka huru watoto wetu katika kutimiza ndoto zao hasa wanapokuwa
shuleni” amesema Waziri Dkt. Mwakyembe.
Aidha, Waziri Dkt. Mwakyembe amesema kuwa bidhaa ya taulo hizo alizozindulia leo
ni rafiki kwa mazingira kwa kuwa zinaweza kutunzwa mahali popote na zisiwe na
madhara kwenye mazingira kwa kuwa haina mchanganyiko wowote wa plastiki. Taulo
hizo zinazotengenezwa na kikundi cha wanawake 12 kiachojulikana kama timu ya
Uhuru Kit Ltd ambao wanaunga mkono juhudi za Serikali katika kutunza mazingira kwa
marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini Julai, 2019.
Katika kuhakikisha Tanzania inatumia vema fursa ya ujio wa Mshindi wa Miss World
2018 Vanessa Ponce wa Mexico, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa Serikali itaandaa
ziara maalum kwa Uongozi wa Miss World ukiongozwa na Mwenyekiti na Mwendeshaji
wa Shindano la Miss World Bi Julia Morley kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii
nchini ikiwemo mbuga za Serengeti, hifadhi ya Ngorongoro pamoja na mji wa
kihistoria wa Zanzibar.
“Uwepo wa Miss World 2018 Vanessa Ponce, dunia nzima macho yao yapo hapa nchini,
ni vema kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia ujio wake” amesema Waziri Dkt.
Mwakyembe.
Kwa upande wake Mwenyekiti na Mwendeshaji wa Shindano la Miss World Bi Julia
Morley amesema kuwa amefurahishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali ya
Tanzania ambapo ni mara ya kwanza kwake kuja nchini.
“Nimefurahi sana Tanzania ni nchi nzuri, nilipopanda ndege kuja hapa nilipata
matangazo yanayosisitiza marufuku ya kutumia mifuko ya plastiki, Serikali imefanya
vizuri kujali kutunza mazingira” alisema Bi Julia Morley.
Nao Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico pamoja na Miss Tanzania 2019
Sylivia Sebastian wamesema kuwa urembo ni heshima, UhuruPads zitawasaidia wasichana kupata elimu wakiwa huru wakizingatia kauli mbiu ya ‘Uzuri wenye
malengo.’
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti na Mwendeshaji wa shindano la Miss World
Bi Julia Morley, Mshindi wa Miss World 2018 Vanessa Ponce kutoka Mexico, Mshindi wa
Miss Tanzania 2019 Sylivia Sebastian Bebastian Bebwa pamoja, mwandaaji wa
Mashindano ya Miss Tanzania Bi. Basilla Mwanukuzi pamoja na walimu na wanafunzi
wa shule ya sekondari Moshono ya jijini Arusha.