SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemuidhinisha Mrundi, Etienne Ndayiragijje kuwa kocha Mkuu rasmi wa timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars.
Taarifa ya TFF usiku huu imesema kwamba TFF imempa mkataba wa mwaka mmoja Ndayiragije, ambaye amekuwa akisaidiwa na wazalendo Suleiman Matola na Juma Mgunda.
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ambayo imezingatia mapendekezo ya Kamati ya Ufundi ya TFF iliyopitia wasifu wa makocha mbalimbali walioomba nafasi hiyo.
Na TFF imevutiwa na kazi nzuri ya Ndayiragije wakati akiwa kocha wa muda tangu Julai mwaka huu alipoiwezesha Taifa Stars kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.
Pamoja na kuipeleka Taifa Stars, michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, pia Ndayiragije ameiwezesha Tanzania kuingia hatua ya makundi katika kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 Qatar.
Taifa Stars ilifanikiwa kukata tiketi ya CHAN ya mwakani nchini Cameroon baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Sudan wiki iliyopita Uwanja wa Omdurman, Mourada mjini Omdurman.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars ikafuzu kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla ya 2-2, kufuatia kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam.
Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Taifa Stars kufuzu fainali za michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, baada ya mwaka 2009 nchini Ivory Coast, ikiitoa Sudan pia katika raundi ya mwisho ya kufuzu.