*********************************
Na Farida Saidy – Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuthubutu kutekeleza kwa Vitendo mradi wa kufua Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Mhe. Loata ametoa pongezi hizo Oktoba 25 mwaka huu alipotembelea mradi wa kufua Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere {Julius Nyerere Hydropower Project – JNHPP}ikiwa ni mara yake ya kwanza kutembelea mradi huo akiwa Mkuu wa Mkoa huo.
Akiambatana na Wajumbe wake wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo ikiwa ni mwendelezo wa ziara aliyoianza hivi karibuni ya kujitambulisha rasmi Mkoani humo pamoja na kuona utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Mhe Ole Sanare anafika katika mradi wa kufua umeme na kujionea kazi inavyoendelea bila kutegemea anajikuta anampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uthubutu wa kutekeleza mradi huo mkubwa na wa thamani utakaowaletea maendeleo wananchi hususan wanyonge.
“kikubwa kuliko yote ni kumshukuru sana na kumpongeza mheshimiwa Rais wetu kwa kutekeleza mradi huu ambao ulishaibuliwa enzi za Mwalimu Nyerere lakini haukuweza kutekelezwa sasa amekuja yeye amesema ni ‘take Off’ sasa (nianze kutekeleza) ni mradi wa siku nyingi sana…” alisema Ole Sanare.
“tumpongeze na kumshukuru sana kwa kufuata nyayo za baba wa Taifa hili yeye amesema yale yote ambayo aliyabuni atayatekeleza na yanatekelezeka” amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Aidha, amewataka wahandisi wazawa wanaosimamia utekelezaji wa mradi huo ambao wanafikia asilimia tisini ya wahandisi wote wanaofanya kazi katika mradi huo, kusimamia kwa uadilifu mradi huo na kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Pamoja na pongezi hizo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameweka wazi kuwa Ofisi yake iko tayari kushirikiana kwa karibu na wakandarasi na wahandisi wa mradi kwa huo kila changamoto itakayojitokeza ili mradi huo ukamilike kwa wakati na kwa malengo yanayotarajiwa.
Pamoja na kukiri kasi nzuri ya mradi huo, Mhe. Ole Sanare ameahidi Kamati yake ya Ulinzi na Usalama itaweka ratiba ya kuutembelea mradi huo kila baada ya miezi miwili ili kujiridhisha kazi inavyoendelea pamoja na kuimarisha Amani ya eneo nzima la mradi.
Katika hatua nyingine Mhe. Ole Sanare wakati wa ziara hiyo alisimama kwa muda eneo la Kisaki ambalo ni kituo kikubwa kilichopo karibu na mradi huo na kutumia dakika kadhaa kuongea na wananchi wa eneo hilo.
Katika hotuba yake amewataka Vijana zaidi ya elfu moja kutoka Mikoa mbalimbali hapa nchini waliofika eneo la Kisaki kwa ajili ya kutafuta kazi kwenye mradi wa bwawa la kufua umeme, kurudi nyumbani kwao ili kutoa nafasi ya eneo la Kisaki kutokuwa na watu wengi kuliko uwezo wake.
Pamoja na agizo hilo kwa vijana kurejea makwao na kurejea hapo watakapohitajika, ameviagiza vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama Mkoani humo kuimarisha Usalama katika eneo la kisaki masaa ishirini na Nne huku akiwataka wanaoshughulika na kupokea vijana kwenye mradi huo kutenda haki katika kuwapokea vijana hao.
Naye Mratibu wa Mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere Mhandisi Stephen Manda ameeleza hatua ya mradi huo akibainisha kuwa wako ndani ya ratiba lakini pia kazi nyingine ziko mbele ya wakati. Amesema lengo lao ni kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa yaani mwezi Juni 2022.
Hata hivyo amewaomba wadau wanaofanyakazi nao na watanzania wote kwa jumla kutoa ushirikiano wa kutosha kwao ili watekeleze kazi hiyo kwa wakati huku akitoa wito kwa Wakuu wa Mikoa ya Morogoro na Pwani ambayo mradi huo upo kuendelea kusimamia suala nzima la Amani ili wafanyakazi wanaofanya kazi katika mradi huo wafanye kazi zao kwa ufasaha na ufanisi.
Kwa upande wake Onesmo Sanga ambaye ni dereva wa Mitambo mikubwa anayetafuta kazi katika eneo hilo la mradi wa kufua umeme, ameiomba Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa – NIDA kuwasaidia kupata namba za vitambulisho ili ziwasaidie kupata kazi katika mradi huo kwa kuwa wengi wao hadi sasa hawana vitambulisho hivyo na kuwa moja ya changamoto kubwa katika kupata kazi.