Mwananchi wa Newala,Shadrack Ntesi akimuuliza swali Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni(hayupo pichani), wakati wa Mkutano wa Hadhara uliofanyika leo katika Stendi ya Mabasi wilayani hapo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni akizungumza katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Stendi ya Mabasi wilayani Newala leo, ambapo ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata Viongozi wa Vyama Vya Msingi vya Ushirika ambao wametoroka na fedha za wakulima wa korosho wilayani hapo,Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Newala Aziza Mangosongo .Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni akisalimiana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Newala baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazi,Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Aziza Mangosongo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
*****************************************
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara kuwakamata Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika wanaotuhumiwa kukimbia na Kiasi cha Shilingi Bilioni 1.2/= za wakulima ambazo ni madeni ya Korosho.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Newala katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Viwanja vya Stendi Kuu baada ya kupokea Ripoti ya Jumla ya Madeni wanayodai wakulima katika Wilaya za Mtwara, Masasi, Nanyumbu, Newala na Tandahimba.
“Nilivyofika hapa Mtwara jambo la kwanza lilikuwa kumuuliza Kamanda wa Polisi wa hapa juu ya utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais alilolitoa siku za hivi karibuni alipokuwa ziara na kuagiza kukamatwa kwa viongozi wawili wa vyama vya msingi vya ushirika wanaodaiwa fedha za korosho na wakulima, ameniambia walitekeleza agizo na hao viongozi wawili tayari wameanza kulipa hizo fedha,” amesema Masauni
Akizungumza baada ya kupokea ripoti ya madeni kwa Wilaya zote za Mkoa wa Mtwara Naibu Waziri Masauni amelitaka Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wengine katika wilaya zilizobakia za Mtwara, Newala, Masasi, Nanyumbu na Tandahimba ambazo katika taarifa ya jumla ya mkoa inaonyesha takribani Shilingi Bilioni 1.2 bado zinadaiwa na wakulima hao kutoka kwa viongozi wa vyama hivyo.
“Mheshimiwa Rais kwenye ziara yake aliishia wilaya ya Masasi lakini katika ripoti hapa inaonyesha katika wilaya zingine wakulima pia wanadai fedha zao ambacho ni kiasi kikubwa,nakuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara kuwakamata viongozi wengine katika wilaya zilizobakia na hakikisha kiasi hicho cha fedha cha wakulima hao kinalipwa,” amesema Masauni
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara,Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Blasius Chitanda inaonyesha jumla ya Vyama vya Ushirika 61 bado vinadaiwa na wakulima katika wilaya za Mtwara, Masasi, Tandahimba na Newala kuanzia Msimu wa Korosho wa Mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano huo baadhi ya wakulima wanaodai fedha zao waliiomba serikali kuhakikisha wanalipwa haki yao kwani madeni hayo yamechukua muda mrefu hali inayopelekea kuzorotesha shughuli zao za kuchumi huku familia zao zikipata taabu kutokana na fedha zao kutopatikana kwa wakati.