Home Mchanganyiko MBUNGE DITOPILE KUJENGA UZIO WA SEKONDARI YA DODOMA

MBUNGE DITOPILE KUJENGA UZIO WA SEKONDARI YA DODOMA

0

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZAZI nchini wametakiwa kushirikiana na Walimu ili kuweza kufuatilia maendeleo ya watoto wao mashuleni na siyo kuacha kila kitu kufanywa na walimu.

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Viti Maalum Taifa anayewakilisha vijana (UVCCM), Mariam Ditopile kwenye mahafali ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Dodoma.

Amesema jukumu la wazazi siyo kununua mahitaji ya mtoto tu bali anapaswa kufuatilia maendeleo yake ya kitaaluma na nidhamu na siyo kuwaachia walimu jukumu hilo peke yao.

” Ndugu zangu wazazi jukumu lenu siyo kununua tu sare za Shule na vifaa vingine, fuatilieni maendeleo ya hawa vijana hapa katikati muda ambao wanaenda na kurudi shule.

Hakuna mtoto anaezaliwa bila akili, wote hawa wana akili tena nyingi sana. Ni jukumu letu sisi wote wazazi, wadau na walimu kulinda uwezo wa watoto wetu, tuhakikishe wanapata elimu na kufuatilia maendeleo yao. Tusiruhusu mitaa ikalea watoto wetu, tukisharuhusu hali hiyo mjue ni ngumu kupata ufaulu Mzuri,” Amesema Ditopile.

Akizungumzia changamoto ya maji na uzio katika Shule hiyo Mhe Ditopile ameahidi kutoa mifuko 50 ya Saruji pamoja na Tenki kubwa la kuhifadhia Maji ndani ya Siku tatu ujenzi wa uzio uwe umeshaanza ambapo yeye mwenyewe pia atatafuta nguvu kazi ya kuja kujenga.

Amesema ni jukumu lao kama wasaidizi wa Rais Dk John Magufuli kumsaidia katika changamoto nyingine na wala siyo kukaa na kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu ilihali wao wenyewe wanaweza kuhamasishana na kumaliza changamoto hizo.

Kuhusu kiwango cha ufaulu shuleni hapo, Mbunge Ditopile ameonesha kukerwa na matokeo ya miaka mitatu ya nyuma ambapo kiwango cha daraja la nne na sifuri kilikua kikubwa kulinganisha na madaraja ya ufaulu.

” Hapa kwenye ufaulu kwa kweli siridhishwi napo, Dodoma Sekondari iko katikati ya Jiji tena Makao Makuu ya Nchi hamuoni tunajipa aibu hii? Hapa hakuna changamoto ya walimu wala vifaa ya kufundishia, kila kitu kipo sasa tatizo ni nini?

Kitendo cha kushindwa kufuta zero shuleni kwetu hapa ni kujinyima fursa za kimaendeleo ambazo Serikali inazileta Dodoma. Fursa kubwa ya elimu ipo Dodoma ni wakati wetu wa kuamka na kujipanga ili kumaliza changamoto hii,” Amesema.

Amewataka wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne kutuliza akili watakapoingia kwenye vyumba vya mtihani ili waweze kufanya vizuri ili kumuunga mkono Rais Magufuli ambaye amewalipia ada kwa miaka yote minne ya masomo yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Father Chesko Kusaga ameishukuru Serikali kwa kuendelea kufanya uwekezaji kwenye sekta ya elimu ambapo tayari walishapokea kiasi cha Shilingi Milioni 900 kwa ajili ya maboresho ya elimu.

” Mhe mgeni rasmi tunakuahidi kuwa tutafuta hizi zero, mwaka huu tumejipana kuhakikisha Dodoma Sekondari kweli inabeba taswira ya Makao Makuu ya Nchi kwa kufanya vizuri kwenye elimu. Hatutomuangusha Rais wetu katika hili.

Lakini pia tuishukuru Wizara ya Elimu kwa kuwa mstari wa mbele kufanikisha maendeleo ya Shule yetu, Tulipokea kiasi cha Shilingi Milioni 195 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na mabweni mawili. Pia tunaishukuru Halmashauri ya Jiji kwa kutupatia Shilingi Milioni 120 za ujenzi wa mabweni,” Amesema Father Kusaga.