Sharifa Mussa Mkazi wa kitongoji cha Chanika akimuonesha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi madai yake ya fidia ya ardhi ambayo bado hayajalipwa wakati wa mkutano wa hadhara wa utatuzi wa kero za ardhi kwa wakazi wa mji wa Handeni katika uwanja wa Soko la Zamani Chanika maarufu Nyerere Square Wilayani Handeni Mkoani Tanga.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe akimpa taarifa ya Wilaya ya handeni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuhusu sekta ya ardhi katika Wilaya yake.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe akimpa taarifa ya Wilaya ya handeni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuhusu sekta ya ardhi katika Wilaya yake.
********************************
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameziagiza Halmashauri za Miji pamoja na watu wenye mashamba makubwa wahakikishe wanawalipa fidia Wananchi wote ambao hawajalipwa kwa muda mrefu tangu kufanyika kwa tathmini kwani wananchi wengi wamekuwa wakiishi ndani ya mashamba yao kwa muda mrefu na wakiamishwa hawalipwi fidia zao kwa miaka mingi na wengine kuondolewa bila kulipwa kabisa.
Waziri Lukuvi meyasema hayo alipofanya ziara Wilayani Handeni Mkoani Tanga wakati wa kusikiliza kero za wananchi katika uwanja wa Soko la zamani Chanika maarufu Nyerere Squre Katika mkutano huo Waziri wa Ardhi aliongozana na Mkuu wa Wilaya hiyo Godwin Gondwe akiwa pamoja na Mbunge wa Jimbo la Handeni Mhe. Omari Abdallah Kigoda na watendaji mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Kupitia kampeni yake ya “FUNGUKA KWA WAZIRI” Mhe. Lukuvi amesikiliza kero za ardhi za wananchi zaidi ya 200 wa wilaya ya Handeni zilizowasilishwa kwake. Kampeni hiyo iliyoanza saa 4 asubuhi hadi saa 12 jioni ambapo wakazi wengi wa mji huo wamelalamikia suala la kulipwa fidia ndogo au kutokulipwa fidia zao kabisa.
Mh. Lukuvi amesema Halmashauri nyingi zimekuwa na pupa za kupanga viwanja bila kuwalipa wananchi fidia na hata ikitokea wakalipa fidia basi fidia itakuwa ndogo sana kwani kwa kufanya hivyo kutazidisha migogoro mingi ya ardhi isiyo ya lazima, hivyo amezitaka halmashauri kupitia upya madai ya wananchi na kuwalipa stahiki zao.
”Kwa kuwa hapa sasa mashamba mengi ya mji huu yamegeuka kuwa ni miji, lazima hawa watu muwafidie viwanja zaidi kuliko pesa kama wanataka pesa basi wauze wenyewe hivyo viwanja, hamuwezi kuwapa shilingi milioni tatu wakati nyinyi mnauza viwanja milioni kumi. Kumekuwepo na unyang’anyi na kuwalazimisha watu kupima viwanja kwa fidia kidogo. Na kwa mujibu wa sheria ya fidia kama hujamlipa mwananchi kwa miaka zaidi ya miwili basi inatakiwa ufanye tathmini upya”.
Hata hivyo Mh.Lukuvi ameshangazwa na wingi wa migogoro ya Ardhi ambayo ilikwisha patiwa ufumbuzi wake na mingine ilikwisha tolewa hukumu na Mahakama lakini cha kushangaza bado wananchi wanacheleweshewa haki zao hivyo kuwaamuru Maafisa ardhi kuhakikisha wanashughulikia swala hilo haraka iwezekanavyo kwani asingependa kuona swala hilo likijirudia tena.
Mhe. Lukuvi amesema kuwa amebaini 90% ya Wananchi wa Handeni hawana uwelewa juu ya hatimiliki ya ardhi zao wanazomiliki kwani ameshangazwa sana kuona wengi wao hawafahamu mipaka ya maeneo yao hali inayopelekea kuzuka kwa migogoro ya mipaka hivyo amewaasa wananchi kuyafatilia maeneo yao na kuyapatia hati miliki ili kuyalinda na wavamizi kwani Hati ndio kielelezo namba moja kinachotambulika kisheria.
“mimi kama Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ipo migogoro ambayo nina uwezo wa kuitafutia ufumbuzi kutokana na mamlaka niliyonayo na ndio maana nimeamua kuwa na kampeni ya Funguka kwa Waziri ili kusikiliza kero mbalimbali za Ardhi lakini hii migogoro ya mtu na mtu inatakiwa kutafutiwa ufumbuzi ndani ya ofisi zenu za ardhi au wilaya” Amesema Waziri Lukuvi.
Hata hivyo baada ya kusikiliza kero za wananchi Waziri Lukuvi ameahidi kuanzisha Baraza jipya la Ardhi na Nyumba la Wilayani Handeni kwani wananchi wamekuwa wakisafiri hadi Wilayani Korogwe kusikiliza mashauri yao jambo ambalo limekuwa na ucheleweshaji wa kusikiliza na kutatua kero za ardhi kwa wakati kwani ndio chanzo cha migogoro mingi Wilayani hapo.
Aidha, akifunguka mbele ya Waziri Bi. Telessa Petro Gumbo ambae ni mkazi wa Handeni amelalamikia uvamizi wa uliofanywa katika shamba lake ambapo amemuomba Waziri Lukuvi kuingilia kati swala lake la kutolulipwa fidia baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kulimega eneo lake na kupitisha barabara hali inayomlazimu kulipwa fidia ya eneo hilo.
Naye, Bi. Amina Ali Kiale ambae pia ni mkazi wa Handeni amemlalamikia Waziri lukuvi kwa baadhi ya watendaji wa Ardhi ambao sio waaminifu kushiriki katika vitendo vya kudhurumu ardhi kwa kuwacheleweshea hati zao kwa muda mrefu wanapokuwa wanazifatilia.
Katika kutoa shukurani kwa Mhe. Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe amemshukuru Mh. Lukuvi kwa kitendo cha kuifanya programu hiyo ya FUNGUKA KWA WAZIRI katika Wilaya yake ya Handeni kwani imeweza kutatua migogoro ya ardhi iliyodumu muda mrefu na kuahidi kushughurikia migogoro iliyobaki katika ofisi yake ya Wilaya.