Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Diana Masalla akizungumza wakati wa Jukwaa la Biashara na Uchumi lililofanyika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu lenye lengo la kujadili fursa, changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wilayani humo.
Washiriki wa Jukwaa la Biashara na Uchumi lililofanyika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu wakisikiliza kwa makini mada mbalimbali zilikokuwa zikiwasilishwa wakati wa jukwaa hilo lenye lengo la kujadili fursa, changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wilayani humo.
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Diana Masalla akizungumza wakati wa Jukwaa la Biashara na Uchumi lililofanyika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu lenye lengo la kujadili fursa, changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wilayani humo.
***********************************
Na Veronica Kazimoto
Simiyu
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Diana Masalla amesema kuwa, mwananchi yeyote atakayefichua wakwepa kodi na TRA ikafuatilia na hatimaye kodi hiyo ikagundulika ni kweli ilikuwa imekwepwa na ikakusanywa, mwananchi aliyetoa taarifa hizo za ukwepaji kodi atalipwa asimilia 3 ya kodi iliyokusanywa lakini haitazidi shilingi milioni 20.
Masalla ameyasema hayo wakati wa Jukwaa la Biashara na Uchumi lililofanyika katika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu ambalo lengo lake ni kujadili fursa, changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara na wawekezaji wilayani humo na kuzitafutia ufumbuzi.
“Natoa wito kwa wananchi na washiriki wa jukwaa hili kuhakikisha mnawafichua wakwepa kodi wote kwa sababu watu hao wanaiibia Serikali yetu mapato na wanarudisha nyumba jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wake,” Amesema Masalla.
Aidha, Masalla amewahimiza wafanyabiashara na wawekezaji walioshiriki jukwaa hilo kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa pindi wanapokuwa wamefunga biashara kutokana na sababu mbalimbali ili kuepuka kuendelea kutozwa kodi au kuonekana wamekaidi kulipa kodi.
“Ni muhimu kutoa taarifa TRA pale ambapo mfanyabiashara amefunga biashara yake lakini pale anapofungua ni muhimu pia kuitaarifu TRA ili kuepuka kuendelea kutozwa kodi unapofunga biashara na pia kuanza kutozwa kodi sahihi pale unapofungua biashara,” amesisitiza Masalla.
Naye, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Wilaya ya Busega David Mateko amempongeza Meneja wa TRA Mkoa wa Simuyu kwa kutoa elimu ya kodi kwa makundi mbalimbali ya wafanyabiashara mkoani humo pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na hatimaye kuifanya Wilaya ya Busega kuwa wilaya ya pili kati ya wilaya 5 za mkoani Simiyu kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yanayosimamiwa na TRA.
“Nampongeza Meneja wa TRA katika Mkoa wetu wa Simiyu kwa kuwatembelea wafanyabiashara na kuwapatia elimu ya kodi na pia nachukua fursa hii kumpongeza Mkuu wetu wa Wilaya Mheshimiwa Tano Mwera kwa kutuhamasisha kulipa kodi kwa wakati na sasa wilaya yetu imekuwa ya pili hapa mkoani kwa ukusanyaji Mapato yanayosimamiwa na TRA,” alibainisha Mateko.
Jukwaa hili la biashara na uchumi wilayani Busega limewakutanisha wafanyabiashara na wawekazaji zaidi ya 200 ambapo taasisi mbalimbali za Serikali zimealikwa kutoa mada ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania.