Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt Faustine Ndugulile akisisitiza jambo kwa baadhi ya Watendaji wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) leo Bungeni Jijini Dodoma baada ya wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Oktoba 23, 2019 Bungeni Jijini Dodoma baada ya kikao na Kamati hiyo.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Oktoba 23, 2019 Bungeni Jijini Dodoma.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakimsikiliza Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe hao leo wakati wa kikao cha Kamati hiyo Bungeni leo Oktoba 23, 2019 Jijini
Dodoma.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo kwa Naibu wake Dkt. Faustine Ndugulile mara baada ya Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Oktoba 23, 2019 Bungeni Jijini Dodoma.
(Picha zote na MAELEZO)
*****************************
Na Mwandishi Wetu
Serikali imewataka wananchi kuepuka matumizi ya dawa zinazotangazwa kupitia mitandao ya kijamii kwa kuwa hazijadhibitishwa ubora wake na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Akizungumza Jijini Dodoma mara baada ya kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Oktoba 23, 2019 Bungeni Jijini Dodoma, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa kumekuwa na wimbi la watu mbalimbali wanaotoa kiholela matangazo ya kuuza dawa za aina mbalimbali kupitia mitandao husika.
“Jamii itambue kuwa kuuza dawa ambazo hazijazidhitishwa ni kosa kisheria na
niwatake wahusika kuacha mara moja kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao”Alisisitiza Mhe Ummy.
Akifafanua, Mhe. Ummy amesema kuwa ifahamike kuwa dawa siyo kama nguo,viatu ama bidhaa nyingine kama hizo ambazo mtumiaji anaweza kununua kadiri utakavyo kutokana na mahitaji au uwezo wake,lakini dawa isiyothibitishwa na mamlaka ni sumu na kwamba inaweza kumgharimu maisha mtumiaji anayetumia bila maelekezo ama ushauri wa daktari.
Aliongeza kuwa, Kamati hiyo imeitaka Wizara yake kuongeza jitihada katika kuzuia matangazo yanayotolewa kupitia mitandao ya kijamii yakinadi dawa za aina mbalimbali ikiwemo kuhusu masuala ya uzazi na magonjwa mengine.
Aidha Mheshimiwa Ummy Mwalimu,amesema,tayari Wizara yake imeshaanza kuchukua hatua kupambana na vitendo vya kutangaza dawa na chakula mitandaoni bila kusajiliwa na kwamba tayari mtu mmoja ameshakamatwa na wakati wowote anatarajiwa kufikishwa mahakamani kufutia kitendo chake cha kutangaza dawa ya kuongeza viungo vya wanaume na kudai kuwa Waziri Ummy,alifungua duka husika lililoko Kariakoo,jijini Dar Es Salaam wakati taarifa hizo zikiwa si za kweli.
Katika hatua nyingine, aliwataka wale wote wanaotaka kuuza dawa kufuata taratibu zilizowekwa kisheria kuepuka kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kikao Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii leo Oktoba 23, 2019 Bungeni Jijini Dodoma imepokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).