Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(kushoto) akimkaribisha Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (kulia) jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya uzinduzi wa mradi wa kuziunganisha shule 14 umma za Mkoa wa Tabora katika mtandao wa tovuti.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri(wenye suti ya kijivu) akiwa na Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe (mwenye suti ya bluu ) na viongozi wengine katika picha ya pamoja jana wakati wa ziara ya Waziri ya siku moja ya uzinduzi wa mradi wa kuziunganisha shule 14 umma za Mkoa wa Tabora katika mtandao wa tovuti.
Baadhi ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari wilayani Urambo, Mkoani Tabora wakiwa katika sherehe fupi jana ya uzinduzi wa mradi wa kuziunganisha shule 14 umma za Mkoa wa Tabora katika mtandao wa tovuti.
Mkuu wa Wilaya ya Urambo Angelina Kwingwa akitoa salama fupi jana wakati sherehe fupi za uzinduzi wa mradi wa kuziunganisha shule 14 umma za Mkoa wa Tabora katika mtandao wa tovuti.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akitoa salama fupi jana wakati sherehe fupi za uzinduzi wa mradi wa kuziunganisha shule 14 umma za wilayani Urambo Mkoa wa Tabora katika mtandao wa tovuti.
Picha na Tiganya Vincent
**************************
SERIKALI imewataka wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kusoma kwa wingi masomo ya sayansi ili kuwaweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini na kwendana na mtazamo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuziunganisha shule 14 umma za Mkoa wa Tabora katika mtandao wa tovuti.
Alisema shughuli nyingi za maendeleo nchini zinahitaji matumizi makubwa ya sayansi na hivyo Wanafunzi wengi wakisoma masomo ya sayansi wataweza kusaidia katika ujenzi wa uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kamwelwe aliwataka Wanafunzi wa Sekondari kuacha kupotoshana na kuogopa kusoma masomo ya sayansi kwa madai ni magumu badala yake wanatakiwa kuongeza juhudi ili hatimaye waje wawe wataalamu watakaotoa mchango wao katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini Tanzania.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alisema kwa kutambua umuhimu wa sayansi katika maendeleo ya wananchi katika Mkoa wa Tabora wameazimia kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi wa shule ya Sekondari anakuwa na Komputya mpakato(laptop) ili iweze kumsaidia kijifunza kwa teknolojia ya sasa kupitia tovuti.
Alisema sanjari la azimio hilo kwa upande wa Shule ya Msingi wamepanga kuhakikisha kuwa kila mtoto anamiliki seti ya hesabu (Mathematical Set) ili kuwavutia watoto wengi kupenda somo la hesabu na masomo ya sayansi.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta aliwataka watoto wa kike waliopo katika shule za Msingi na sekondari kutoogopa kusoma masomo ya sayansi kwa kuwa uwezo wanao kama walivyo watoto wa kiume.
Alisema wapo wanawake wengi wako katika nyadhifa mbalimbali za utumishi wa umma wa sekta binafsi wakisimamia vitengo vya uhandisi kwa sababu ya kufanya vizuri katika masomo ya sayansi.
“Mimi ninafurahi ninapowaona watoto wa kike wakifanyakazi za uhandisi na kazi nyingine zinawiana na masomo ya sayansi…mabinti zangu wa Urambo na nyie someni masomo ya sayansi kwa bidi ili nanyi siku moja muwe kama wanawake hao mnawaona wamesoma masomo ya sayansi…wanawake tunaweza someni masomo ya sayansi” alisisitiza.