Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike (kulia) pamoja na Afisa Tarafa ya Dodoma Bi. Neema Nyalege wakishirikiana na baadhi ya wataalam wa Maendeleo ya Jamii na wananchi wa Kata ya Iyumbu kushiriki ujenzi wa Maabara ya Shule ya Sekondari Iyumbu Mkoani Dodoma.
Afisa Tarafa ya Dodoma Bi. Neema Nyalege akikabidhi kiasi cha shilingi Milioni moja kama harambee ya hapo hapo kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Iyumbu kuchangia ujenzi wa maabara ya Shule ya Sekondari Iyumbu Mkoani Dodoma wakati wa zoezi la kuamsha ari ya wananchi kujiletea maendeleo iliyoendeshwa shuleni hapo na wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii Nchini.
Baadhi ya wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii Nchini wakishiriki zoezi la kuamsha ari ya wananchi kujiletea maendeleo iliyofanyika shule ya Sekondari ya Iyumbu leo Jijini Dodoma.
Baadhi ya wataalamu wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii Nchini wakishiriki zoezi la kuamsha ari ya wananchi kujiletea maendeleo iliyofanyika shule ya Sekondari ya Iyumbu leo Jijini Dodoma.
Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Dkt. Bakari George akishiriki zoezi la kuamsha ari ya wananchi kujiletea maendeleo iliyofanyika shule ya Sekondari ya Iyumbu leo Jijini Dodoma na Wataalam wa Maendeleo ya Jamii.
Baadhi ya wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii Nchini wakishiriki zoezi la kuamsha ari ya wananchi kujiletea maendeleo iliyofanyika shule ya Sekondari ya Iyumbu leo Jijini Dodoma.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
…………………
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike amesema kimsingi jukumu la wataalam wa Maendelaeo Nchini sio tu kutoa mikopo kwa vikundi vya uwezeshaji wananchi kiuchumi bali ni kuchechemua ari ya wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Bw. Golwike amesema hayo Mkoani Dodoma katika Kata ya Iyumbu wakati wa zoezi la wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii kushiriki ujenzi wa maabara ya Shule ya Sekondari Iyumbu iliyoko nje kidogo ya Jiji la Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa Wiki ya Mkutano Mkuu wa wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii.
Bw. Golwike ameviambia vyombo vya habari kuwa ushiriki wa zoezi la ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara ya shule hiyo endeshwa na wataalam wa sekta ya maendeleo ya jamii ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996 kwa vitendo kwani sera hiyo inawataka wananchi kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Naye Afisa Tarafa ya Dodoma Bi. Neema ambaye alisoma hotuba yake kwa wataalam hao kumwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Bw. Patrobas Katambi amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhamasisha jamii kujiletea maendeleo bado mwamko wa jamii kutumia rasilimali zilizopo kujiletea maendeleo bado huko chini.
Bi. Neema aliongeza kuwa kwa wataalam hao kutambua mwitikio huo mdogo kwa jamii ndio maana wameamua kushirikiana na wananchi wa kata ya Iyumbu kujenga maabari hiyo ya vyumba vitatu ili kuamsha ari ya wananchi kushiriki kujiletea maendeleo.
Bi. Neema aliitaja hatua hiyo kuwa ya kupongeza kwani imetekeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996 inayohimiza wananchi kujiletea Maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Aidha Bi. Neema amewataka wanafunzi shuleni hapo kusoma masomo ya Sayansi ndio maana wataalam hawa wako hapa ili kuchangia ujenzi wa maabara yao kwa lengo la kuwapa hamasa wanafunzi shuleni hapo kusoma sayansi kwa vitendo badala ya nadharia ili hapo baadae waweze kulisaidia taifa katika fani ya sayansi na teknolojia.
Aidha Bi. Neema amepongeza jitihada zilizofanywa na uongozi wa chama cha taaluma ya Maendeleo ya Jamii maarufu CODEPATA kwa kujitolea ujenzi wa vyumba vya maabara lakini pia kutoa mifuko ya saruji 120 kwa ajili ya ujenzi wa maabara hiyo itakayogharimu kiasi cha takribani milion 200 mpaka kukamilika kwake.
Mtendaji wa kata ya Iyumbu Bw. Vicent Leo ameitaja Kata yake kuwa moja ya Kata 41 zinazounda Jiji la Dodoma yenye wakazi elfu 6.5 hivyo kuongeza kuwa ujenzi wa Sekondari Iyumbu haukwepeki ili kupunguza hadha ya wanafunzi kwenda mwende mrefu kufuata elimu mbali na Kata yake.
Bw. Leo amezitaja gharama za ujenzi wa Maabara hiyo kuwa ni gharama ya takriban milioni 200 mpaka sasa kiasi cha fedha ambacho kimetumika ni shilingi milioni 32 ikiwemo michango ya wananchi pamoja na fedha kutoka ofisi za kata hiyo .
Wakati huo huo Rais wa Chama cha Wataalam wa fani ya Maendeleo ya Jamii Nchini Bw. Sunday Wambura wakati akiongea na wananchi wa kata ya Iyumbu pamoja na wataalam wenzake amesema kazi ya wataalam wa maendeleo ya jamii ni kukaa na kula na wananchi na baadae kufanya kazi pamoja nao kufanya kazi lengo la kujiletea maendeleo.
‘’Dhana kubwa ya maendeleo ya jamii ni kuamsha hari ya wananchi kujiletea maendeleo na unaweza kuona kama hatujafanya kitu sana lakini tumeokoa shilingi milioni sita ambazo wananchi wa kata hii wangelazimika kuzitumia ili kutekeleza kazi hii’’Aliongeza Bw. Wambura.
Naye Mkazi wa kata ya Ijumbu Bi. Janeth David amewashukuru wataalam wa Maendeleo ya Jamii kwa kuja kuwaunga mkono juhudi zaoza kujenga shule na maabara ili kuwakomboa watoto kutembea umbali wa kilometa 24 kufuata huduma ya elimu katika Shule ya Sekondari Kisasa.
Wataalamu wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii wanakutana Jijini Dodoma katika Mkutano Mkuu wao wa mwaka kwa lengo la kukumbushana majukumu yao lakini pia kupata maaraifa mapya kutoka mada mbalimbali zitakazotolewa katika mkutano huo wa siku nne.