Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiwahamasisha jana Madreva wa Bajaji na Bodaboda katika Manispaa ya Tabora kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ili waweze kunufaika na huduma za matibabu.
Meneja wa Bima ya Afya Mkoa wa Tabora Adam Salum akiwaelimisha jana Madreva wa Bajaji na Boda boda wa Manispaa ya Tabora utaratibu wanaotakiwa kuchukua kujiunga na Bima ya Afya ili waweze kupata matibabu pindi wanapokuwa wagonjwa.
Baadhi ya Madreva wa Bajaji na Boda boda na wananchi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora (hayupo katika picha) alipokuwa akiwaeleza umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya.
Picha na Tiganya Vincent
*********************************
NA TIGANYA VINCENT
UMOJA wa Madreva wa Bajaji na Bodaboda Mkoani Tabora wameipongeza Serikali kwa kuwasaidia kuingia katika Mfumo wa kupata huduma za matibabu kupitia Bima ya Afya.
Hatua hiyo itasaidia kuwapa fursa ya kuokoa maisha yao wanapopata matatizo mbalimbali ikiwemo wanapopata ajali na wakati mwingine kuugua.
Kauli hiyo imetolewa jana na Makamu Mwenyekiti wa Madreva Bajaji Waziri Kipusi wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ya kuwahamasisha Madreva Bajaji na Bodaboda kujiunga na Bima ya Afya.
Alisema kabla ya kuanza kwa utaratibu huo haujaanza walikuwa wakilazimika kusema uongo ili wenzao waliopata ajali wapate matibabu.
“Ikitokea mwenzetu amepata ajali na tunaposhindwa kuchangishana ilibidi wakati mwingine tusema uongo ili tumuoke mwezetu aliyepata majanga… na wakati mwingine tuliwadanganya Maafisa Ustawi wa Jamii ili watupe kibali cha kupata matibabu kwa mkopo wa matibabu” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Madreva Bajaji Mkoa Said Maganga alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwawezesha kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wote na kuendelea na shughuli za kujiingizia kipato.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Aggrey Mwanri aliwataka Vijana wote wanaojihusisha na usafirishaji wa abiria kwa kutumia Bajaji na Pikipiki maarufu kama bodaboda kuchangamkia fursa hiyo iliyotolewa kwao na Serikali ya awamu ya tano.
Alisema kupitia utaratibu huo watanufaika kwa kupata huduma za Bima ya afya kwa kuchangia shilingi 100,000/- kwa mwaka badala ya ule wa mtu mmoja kulipa shilingi 1.5 kwa mwaka ili kupata huduma hizo.
Mwanri alisema Serikali imeamua kuwapunguzia mzigo kwa wale Bodaboda na Bajaji ambao watakuwa wako katika umoja ili waweze kupata huduma za afya kwa gharama nafuu.
Naye Meneja wa Bima ya Afya Mkoa wa Tabora Adam Salum alisema siku za nyuma Mfuko wa Bima ya Afya ulikuwa ukihudumia watumishi wa umma pekee lakini hivi sasa umeiongia makundi mbalimbali kama vile Wajasiriamali , Umoja wa Boda boda na Bajaji.