Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga, akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa waandishi wa habari jana, katika kipindi cha Julai-Septemba mwaka huu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga, akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari jana,yaliyolenga utendaji wa taasisi hiyo katika kipindi cha Julai-Septemba mwaka huu.
Waandishi wa habari baadhi wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza Emmanuel Stenga (mwenye tai nyekundu) wakiwemo watumishi wa taasisi hiyo jana.
Picha na Baltazar Mashaka
…………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
TAASISI ya Kupamba na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza imeokoa na kudhibiti upotevu wa fedha zaidi ya sh. milioni 50 mkoani humu huku kati ya fedha sh. milioni 30 zikirejeshwa kwenye akaunti maalumu ya serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkuu wa TAKUKURU mkoani humu Emmanuel Stenga alisema kuwa uokoaji na udhibiti wa upotevu wa fedha hizo ulifanyika katika kipindi cha Julai-Septemba mwaka huu.
“TAKUKURU Mkoa wa Mwanza katika mapambano ya rushwa, udhibiti wa ubadhirifu wa fedha za umma kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, 2019 imefanikiwa kuokoa sh.42,529,840 na kudhibiti upotevu wa sh.8,294,560.Kati ya fedha hizo sh.30,206,840 zemerejeshwa BOT kwenye akaunti maalumu ya serikali,’alisema Stenga.
Alisema kiasi kingine cha sh.11,413,000 zilizobainika kufanyiwa ubadhirifu kwenye mradi wa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Salongwe wilayani Magu pia kimerejeshwa kwenye akaunti ya serikali ya kijiji hicho.
Pia Stenga alisema, sh. 640,000 zimerejeshwa baada ya ukaguzi wa taasisi hiyo kufanyika kwenye mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Kakerege wilayani Ukerewe baada ya kubainika kuwa madirisha yaliyowekwa kwenye vyoo vya shule hiyo kutolingana na thamani ya fedha iliyolipwa.
Aidha, taasisi hiyo ilikagua miradi nane ya maendeleo katika sekta za elimu, maji na afya yenye thamani ya sh.2,152,600,000 ili kuona fedha za serikali zinatumika kwa usahihi na miradi inatekelezwa kwa kiwango kinachotakiwa kulingana na thamani ya fedha.
Stenga alifafanua kuwa kati ya miradi iliyokaguliwa sita ni yelimu yenye thamani ya sh. milioni 806.6, maji mradi mmoja wenye thamani ya milioni 986 na afya wenye thamani ya sh. milioni 360 na walifuatilia na kukagua fedha za ruzuku zinazotolewa na serikali kwa shule za msingi ambapo 70 zilikaguliwa katika halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza.
“Lengo kuu la ufuatiliaji huu kwenye miradi inayotekelezwa, ni kuzuia mianya ya rushwa na upotevu wa rasilimali ama kudhibiti fedha za serikali inapobidi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ili itekelezwe kwa kiwango kinachotakiwa na thamani ya fedha ionekane,”alisema Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoani humu