Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) imekuwa na utaratibu wa kuandaa Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo kila mwaka. Tamasha la mwaka huu ni la 38 na litaadhimishwa kuanzia tarehe 19 hadi 26 Oktoba, 2019 katika mji wa kihistoria wa Bagamoyo. Bagamoyo ni moja ya Maeneo yenye Urithi na utajiri mkubwa wa ukitamaduni Ulimwenguni. Aidha, Tamasha hili litafanyika katika viwanja na kumbi za Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).
Shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika wiki nzima ya Tamasha itakua ni pamoja na maonyesho ya sanaa za jukwaani, maonyesho ya sanaa za ufundi, filamu, warsha na makongamano mbalimbali yatakayohusisha wasanii na wadau wa sanaa kutoka ndani na nje ya Tanzania husani Marekani, Finland, Botswana, Kenya, Korea Kusini, Zimbabwe, Mayotte, Uganda na Zambia.
Katika wiki ya tamasha zipo siku ambazo zitakua maalum kwa ajili ya ratiba mahsusi.
Jumapili tarehe 20.10.2019 itakuwa siku ya muziki wa taarabu, Jumatatu tarehe 21.10.2019 itakuwa siku ya filamu na Jumatano tarehe 23.10.2019 ni siku ya muziki wa dansi.
Baadhi ya wasanii wa ndani wanaotarajiwa kushiriki katika tamasha ni: Mwana FA, Juma Nature, Barnaba, Dullar Makabila, Gigy Money, Vitalis Maembe, JhikoMan & Afrikabisa Band, Mashauzi Classic, Hadija Kopa, Thabit Abdul, Msondo Ngoma, John Kitime & JFK Band, Sisi Tambala, Sinaubi Zawose, Shada Acrobatics, Ngome Magic Show JWTZ, Kikundi cha Sanaa cha Taifa Zanzibar, Chuo cha Polisi Moshi, Bagamoyo Players, na vingine vingi.
Tamasha la 38 limebeba kaulimbiu ya “Sanaa na Utamaduni Ajira Yangu” ikiwa imelenga kuwahimiza vijana kufanya sanaa ajira rasmi ambayo inaweza kuwaingizia fedha na kukuza kipato chao na hatimaye kuongeza pato la nchi kwa ujumla.
Mgeni Rasmi wakati wa ufunguzi wa Tamasha la 38 atakua Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Harrison G. Mwakyembe (Mb.).
Tamasha linatarajia kufikia tamati kwa kufungwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Juliana D. Shonza (Mb.).
Lengo kuu la Tamasha hili ni kuendeleza na kudumisha Utamaduni wa Mtanzania, kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa mataifa mengine kupitia warsha, kongamano na maonyesho mbalimbali. Kusudi la Tamasha vile vile ni kutoa fursa kwa wasanii wa ndani na nje ya nchi pamoja na watazamaji kukutana na kuuenzi utajiri wa utamaduni wao unaowatofautisha na mataifa mengine ambao unaonyesha utofauti wao katika muktadha wa maadili na mshikamano pamoja na ubunifu.
Ni jukwaa kwa wanafunzi wa TaSUBa na wa kutoka taasisi zingine za mafunzo kuonesha kazi zao na stadi walizopata katika mafunzo yao ya sanaa na utamaduni.
Tamasha ili ni jukwaa la wasanii wachanga kuonesha vipaji vyao na ustadi wao kwenye sanaa na utamaduni. Vile vile linaongeza uhamasishaji miongoni mwa vijana na wasanii juu ya maswala yanayohusu sanaa, michezo na utamaduni wa Kitanzania.
Mwaka huu, Tamasha linatarajia kuhudhuriwa na jumla ya watazamaji kati ya 60,000 hadi 100,000 kutoka maeneo ya Bagamoyo, Dar es salaam na sehemu zingine za Tanzania pamoja na nje ya Tanzania.
Aidha, kutakua na maonesho ya bidhaa mbalimbali za sanaa na za kiutaamaduni, vyakula mbalimbali kama vile nyama choma, samaki, pamoja na vyakula vya baharini. Aidha, wageni watapata fursa ya kutembelea mji wa kihistoria wa Bagamoyo na kijifunza mengi kuhusu utamaduni na mambo mbalimbali ya kihistoria.
Mwisho, TaSUBa inawakaribisha wadau mbalimbali wa sanaa pamoja na wananchi kwa ujumla kuhudhuria tamasha hili la kihistoria. Pia tunatoa fursa kwa wajasiriamali kuja kuonyesha na kuuza bidhaa zao mbalimbali.