Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula Akizungumza na viongozi wa wilaya ya Ukerewe pamoja na Watumishi wa Shamba la Miti la Rubya katika wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za watumishi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jana
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula Akielekea kukagua moja ya nyumba za watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika shamba la Misitu la Rubya lililoko Ukerewe wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za watumishi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jana. Wa pili kulia ni Meneja wa NHC Mwanza Fadhili Ntahana na kulia ni Katibu Tawala Wilaya ya Ukerewe Focus Majambi
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula Akielekea kukagua moja ya nyumba za watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika shamba la Misitu la Rubya lililoko Ukerewe wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba za watumishi zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jana. Kushoto kwa Naibu Waziri wa Ardhi ni Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Mwanza na Geita Fadhili Ntahana
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula Akiangalia maendeleo ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika shamba la Misitu la Rubya lililoko Ukerewe wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jana.
………………………
Na Munir Shemweta, WANMM UKEREWE
Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha inalipima na kupatiwa hati shamba lake la Miti la Rubya lenye ukubwa wa hekta 1,926.3 lililopo kijiji cha Bugula tarafa ya Ilangala kisiwa cha Ukerewe mkoani Mwanza.
Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana wakati alipokwenda kukagua ujenzi wa nyumba za watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati akiwa katika ziara yake ya siku moja katika kisiwa cha Ukerewe kufuatilia utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika hamashauri za mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Alisema, kinachohitajika sasa kwa Wakala wa Huduma za Misitu ni kuhakikisha shamba hilo la Miti la Rubya linapimwa na kupatiwa hati itakayoonesha mipaka halisi ya shamba hilo ili kuepuka migogoro ya ardhi.
‘’Miji inakuwa kuwa na wananchi bado wanahitaji maeneo bila kuwa na hati inaoonesha mipaka ya shamba kunaweza kuleta migogoro na tuelewe hati inalinda mipaka ya shamba lisivamiwe na wananchi’’ alisema Dokt Mabula
Pamoja na kuagiza kupimwa hilo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliagiza pia eneo la shamba kuwa Mpango Kina utakaonesha kila matumizi ya sehemu ya ardhi ya shamba hilo kwa kuwa katika eneo hilo mbali na shamba la misitu lakini kuna makazi ya watu.
Kwa upande wake Meneja wa Shamba la Miti la Rubya wilayani Ukerewe Festo Chaula alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba an Maendeleo ya Makazi kuwa, Shamba la Miti la Rubya ni miongoni mwa mashamba 23 yanayomilikwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania lililoanzishwa mwaka 1951 kwa Tangazo la Serikali Namba 230.
Alisema, pamoja na shamba hilo la Rubya pia Wakala inalo eneo lingine lilipandwa miti kwa ubia na halmashauri ya wilaya ya Ukerewe lenye ukubwa wa hekta 1,152 ambapo miti iliyopandwa eneo hilo ni ya Misindano.
Kwa mujibu wa Chaula, katika kuboresha makazi ya watumishi wa wakala wa Huduma za Misitu TFS katika mwaka huu wa fedha 2019/2020 TFS imetenga zaidi ya milioni 383.8 kwa ajii ya ujenzi wa nyumba tatu, tenki la kuhifadhia maji, ukarabati wa nyumba mbili na ujenzi wa uzio wa bustani ya miti ambapo ujenzi wa nyumba tatu ulianza Agosti mwaka huu.
Katika Hatua Nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka halmashauri ya wilaya ya Ukerewe kufanya zoezi la upimaji maeneo katika halmashauri hiyo kama operesheni maalum ili kuondoa migogoro ya ardhi sambamba na kuondoa ujenzi holela.
Akizungumza na Madiwani pamoja na Watumishi wa Sekta ya Ardhi katika halmashauri hiyo, Dkt Mabula alisema tayari halmashauri hiyo inavyo vifaa vya upimaji inachotakiwa kwa sasa katika kuharakisha zoezi hilo ni kuwasiliana na Ofisi ya Ardhi Kanda ya Ziwa kwa ajili ya kupatiwa Wapimaji.
Hata hivyo, Dkt Mabula alishangazwa na halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kutokuwa na kijiji chenye mpango wa matumizi bora ya ardhi wakati asilimia kumi ya kisiwa hicho ni ardhi ya nchi kavu. Halmashauri kerewe ina jumla ya vijiji 73 ambapo Naibu Waziri aliwataka Madiwani wa Halmashauri ya Ukerewe kuhakikisha inapanga mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji vyake ili kuainisha matumizi mbalimbali ya vijiji hivyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe George Nyamaha alieleza kuwa halmashauri yake imekuwa na chanagmoto kubwa ya upungufu wa wataalamu wa sekta ya rdhi jambo alilolieleza kuwa linasababisha idara hiyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.