Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwasalimia wanafunzi wa shule ya Sekondari Bogwe wakati alipowasili shuleni hapo kwa ajili ya mahafali ya 22 ya shule hiyo
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa mahafali ya 22 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Bogwe Kasulu Mkoani Kigoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akipata maelezo ya namna microscope inavyofanya kazi kutoka kwa mmoja wa wanafunzi wa shule ya sekondari Bogwe
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akimtunuku cheti mhitimu wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Bogwe
Wanafunzi wa kidato cha nne shule ta sekondari Bogwe wakifuatilia hotuba ya waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia (hayupo pichani)wakati wa mahafali ya 22 ya shule hiyo
Waziri wa Elimu, Saynsi na Teknolojia prof. Joyce akiteta jambo na Mmoja wa wanafuzi wa kidato cha nne Feodola Binigila anaesoma masomo ya jioni Bogwe sekondari mara baada ya kumtunuku cheti cha ufaulu katika masomo.
……………….
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa siku 14 kwa Kamishna wa Elimu kuhakikisha anawasilisha mapendekezo ya namna ya kurekebisha waraka wa elimu unaoruhusu mwanafunzi awe mtoro bila kutoa taarifa ndani ya siku tisini.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Bogwe iliyoko Halmashauri ya Mji Kasulu mkoani Kigoma ambapo amesema waraka huo hauko sawa na wanafunzi wanautumia vibaya kwa kutokwenda shule jambo linalowapelekea kukosa masomo.
Amesema ni lazima sasa kuwa na mfumo ambao mwanafunzi anapokuwa haonekani shuleni ndani ya muda ambao wataalamu wataona ni muafaka mzazi apate taarifa kwani taratibu zilizopo sasa ni za kuwadekeza wanafunzi.
” Kama mwalimu asipofika shule ndani ya siku tano amejifukuzisha kazi, iweje mwanafunzi siku tisini?uwiano uko wapi? Kamishna hili jambo nimeshalizungumza na umeanza kulifanyia kazi tangu mwezi wa saba. Muda ni mrefu nilizungumza katika kikao cha Wizara. Kamilisha kazi na watendaji acheni uzito, angalia kazi ya Mhe. Rais na mimi Waziri wenu, twende pamoja vinginevyo utakaa pembeni,” aliongeza Waziri Ndalichako.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Bogwe kusoma kwa bidii ili kufuta historia ya matokeo mabaya ya mitihani ya Taifa katika shule hiyo kwani Serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza kwenye miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule nchini ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira mazuri.
“Ukiangalia kwa mfano katika shule yenu hii ya Bogwe Serikali imetoa shilingi milioni 378 ambazo zimejenga miundombinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukumbi ambao mnafanyia mahafali sasa kazi iliyobaki kwenu ni nini? someni kwa bidii hamna cha kulaumu Serikali imetelekeza kazi kwenu sasa,” aliongeza Waziri Ndalichako.
Amewataka wanafunzi hao kuwa mabalozi wazuri na mfano mzuri wa kuigwa mahali popote watakapokuwa ili kuijengea sifa shule waliyosoma na kuwa wazalendo na Taifa ikiwa ni pamoja na kuilinda nchi kwa gharama yoyote.
“Kamwe msikubali kutumika na watu ambao wanataka kuvuruga amani, umoja na mshikamano katika Taifa hili, Muasisi wa Taifa hili Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifanya kazi kubwa kujenga amani, mshikamano na umoja. Tuendelee kumuenzi kwa kuhakikisha tunalinda tunu za Taifa alizoziacha,’alisema Waziri Ndalichako.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange ametoa wito kwa wazazi kote nchini kuzingatia malezi bora kwa watoto wao ili kutengeneza kizazi chenye maadili kitakachosaidia katika ujenzi wa taifa.
Awali, akizungumza katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bogwe David Kindanda alimweleza Waziri Ndalichako shule imetekeleza mikakati ya kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo akiahidi kuongeza bidii na mbinu za ufundishaji ili kuwawezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao akisisitiza kudhibiti utoro na kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike ambao amedai kuwa bado hawafanyi vizuri.
“Pamoja na mikakati hiyo Mhe. Waziri tunaomba sheria inayompa mwanafunzi nafasi kuwa mtoro kwa siku tisini mfululizo ndio afukuzwe shule irekebishwe kama ulivyowahi kusikika ukisema wazi. Sheria hiyo inahitaji marekebisho kwani mwanafunzi hawezi kusomeshwa shule bure halafu kuwa mtoro wakati wapo wanaotafuta fursa na wanaikosa,” alisema Mkuu wa shule ya Sekondari Bogwe.
Akisoma risala ya wahitimu wa Kidato cha nne Shule ya Sekondari Bogwe, mhitimu Faraji Joseph ameishukuru Serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia huku wakiiomba kuwasaidia kupata maji shuleni hapo kwani kwa sasa wanayafuata mto Bogwe jambo ambalo ni hatari kwa wanafunzi hasa wakati wa vumbi la kiangazi.