*************************************
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Mhandisi Zephania Chaula ameagiza vituo vya kuandikisha wapiga kura katika vituo vya vitongoji 24 vya Mji mdogo wa Mirerani kuhamia kwa muda kwenye lango la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite ili kuwapa watu wengi fursa ya kujiandikisha.
Mhandisi Chaula alisema shughuli ya uandijishaji imehamishiwa kwa muda kwenye eneo hilo ila vituo husika vitaendelea na kazi hiyo baada ya kukamilika kwa uandijishaji katika lango hilo.
Alisema tangu asubuhi ya leo wamefanikisha kuandikisha watu 2,111 kupitia vitongoji 24 vya kata mbili za Mirerani na Endiamtu katika mji mdogo wa Mirerani.
“Baada ya kuona shughuli ya uandikishaji inasuasua kwenye mji mdogo wa Mirerani na Orkesumet kamati ya usalama ikaamua kuweka mikakati ya kufanikisha uandikishaji,” alisema mhandisi Chaula.
Alisema hadi hivi sasa watu 81,400 wamejiandikisha wilayani humo kati ya makisio ya wananchi 105,052 wanaotarajiwa kujiandikisha sawa na asilimia 85.
Alisema anatarajia wananchi wengi watajiandikisha na hadi sasa wanatarajia kufikia asilimia 90 na leo watamalizia zilizobakia.
“Nawashukuru wananchi wote kwa kujitokeza kujiandikisha na wasimamizi wa uandikishaji huo kwani agizo la Rais John Magufuli la kutaka wenye sifa washiriki uchaguzi huo linafanikishwa,” alisema mhandisi Chaula.
Hata hivyo, ameagiza vitongoji na vijiji vya wilaya hiyo kufanya mikutano yao siku ya mwisho ya kujiandikisha ili wakamilishe kwa kila mmoja kutumia haki yake ya kujiandikisha.
Mmoja kati ya waliojiandikisha kwenye lango hilo Mohamed Hassan alisema yeye ni mkazi wa Kitongoji cha Zaire na ameshajiandikisha kabla hajaingia ndani ya lango hilo.
“Kuna baadhi ya watu wanaopanda kwenye migodi ya Tanzanite wamepata fursa ya kujiandikisha baada ya mkuu wa wilaya kuagiza shughuli hiyo ifanyike hapa kwa muda,” alisema Hassan.