Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amesema hadi sasa uandikishaji wa orodha ya wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa umefikia watu milioni 16.9 sawa na asilimia 74.
Aidha, Mkoa wa Dar es salaam umeshika nafasi ya kwanza uandikishaji kwa kufikia asilimia 89.
Hayo ameyasema leo ofisini kwake jijini Dodoma alipokutana na waandishi wa , Jafo amesema kumekuwa na hamasa kubwa kwenye uandikishaji baada ya viongozi mbalimbali hususan wakuu wa mikoa na wilaya kuingia mitaani kuhamasisha wananchi.
“Hadi Oktoba 15 baada ya kuongezwa siku moja uandikishaji umefikia watu milioni 16.9 sawa ba asilimia 74 na mikoa yote imeshapita asilimia 50,” amesema
Aidha amebainisha kuwa Mkoa wa Kigoma umefikia asilimia 57, Kilimanjaro asilimia 58, Arusha asilimia 66 na Shinyanga asilimia 66.
Hata hivyo, amesema mikoa inayoshindana kwa kiwango kikubwa ni Dar es salaam asilimia 89, Pwani asilimia 86, Tanga asilimia 81, Mtwara asilimia 80 na Lindi asilimia 77.
Vilevile, Waziri Jafo amesema Halmashauri ya jiji la Arusha ndio pekee ipo chini ya asilimia 50 huku ikifuatiwa na Manispaa ya Moshi ambayo ina asilimia 51 na Korogwe asilimia 51.
“Kuna clip inatembea na waraka mbalimbali hayo sio maelekezo ya Ofisi ya Tamisemi kilichopo ni watu wanahamasisha, na kanuni zipo wazi,”amesema.
Ametoa rai kwa viongozi wa kisiasa kuwa ni vyema wakazungumza ukweli kuliko kupotosha wananchi kwa kuwa uandikishaji wa uchaguzi huo umefanyika vizuri ikilinganishwa na mwaka 2014 ambapo walikuwa watu milioni 11.8.