Home Mchanganyiko NAIBU WAZIRI MABULA ATAKA VIJANA KUJIFUNZA MAISHA YA NYERERE KWA VITENDO

NAIBU WAZIRI MABULA ATAKA VIJANA KUJIFUNZA MAISHA YA NYERERE KWA VITENDO

0

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasha mshumaa katika kaburi la Baba wa Taifa Mawalimu Julius Kambarage Nyerere wakati wa Maadhimisho ya Miaka 20 ya kifo chake katika kijiji cha Mwitongo Butiama mkoa wa Mara leo tarehe 14 Oktoba 2019.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Wa pili kushoto) pamoja na viongozi wengine wakiwa mbele ya kaburi la hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere Maadhimisho ya Miaka 20 ya kifo chake katika kijiji cha Mwitongo Butiama mkoa wa Mara leo tarehe 14 Oktoba 2019. Kulia ni Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba na wa pili kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Phillip Mangula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Wa tatu kulia) pamoja na viongozi wengine wakiwa nje ya Kanisa Katoliki Parokia ya Butiama mara baada ya Misa ya kumuombea Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya kifo chake katika kijiji cha Mwitongo Butiama mkoa wa Mara leo tarehe 14 Oktoba 2019. Wa kwanza kushoto ni Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba na wa pili kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Phillip Mangula. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Sospeter Muhongo na wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).

********************************

Na Munir Shemweta, WANMM BUTIAMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula amewataka vijana kujifunza maisha ya baba wa Taifa Mwalimu Julius kwa vitendo ili matendo ya kiongozi huyo wa kwanza wa Tanzania yaendelee kukumbukwa.

Akiwa katika Maadhimisho ya miaka 20 ya kumbukumbu ya Mwl.  Nyerere katika kanisa Katoliki la Bikira Maria jimbo la Musoma Parokia ya Butiama mkoani Mara leo tarehe 14 Oktoba 2019 Dkt Mabula alisema, ni vyema vijana wa watanzania wakatumia hazina ya wazee kama Mwl Nyerere Julius Nyerere kuwa chachu ya kuishi kwa vitendo.

“Niwaombe vijana kutumia hazina ya wazee wetu na kuwa chachu ya kuishi kwa vitendo” alisema Dkt Mabula.

Dkt Mabula ambaye alikuwa Mkuu wa kwanza wa wilaya ya Butiama mkoani Mara  alihitimisha salamu zake za miaka 20 ya kifo cha Mwalimu Nyerere wilayani Butiama kwa kuwataka wananchi kuishi pia kwa kumcha Mungu kwa kuwa wakati wa uhai wake baba wa taifa aliishi kwa kumcha Mungu. 

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Sinde Warioba alimueleza Mwl Nyerere kuwa alikuwa ni mtu wa maisha ya Mungu aliyejitahidi kujenga umoja na mshikamano kwa nchi yake na Bara la Afrika kwa ujumla.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Phillip Mangula alimuelezea Mwl Nyerere kama mtu aliyepigania haki na aliyesisitiza kuwa binadamu wote ni ndugu na Afrika ni moja.

Maadhimisho ya miaka 20 ya kumbukumbu ya Mwl Nyerere katika kanisa katoliki Parokia ya Butiama mkoani Mara  yalihudhuriwa pia na  Mkuu wa mkoa wa Mara Adam Malima, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM  Steven Wasira, Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Sospeter Muhongo,  Chief Wanzagi,  Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Dkt Maulid Banyani na Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania  Masanja Kadogosa.