RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa Maafisa Wadhamini wanadhima kubwa ya kuwasimamia wale wote wanaovunja misingi ya kukuza uchumi hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo, huko katika ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta na Makonyo Wawi wakati alipokutana na Watendaji na Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na viongozi wa vikosi vya SMZ na SMT wanaofanya kazi zao kisiwani Pemba.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa, kwa mwaka jana kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar ilifikia asilimia 7.1 na matarajio ni kukua kwa uchumi huo mwaka hadi mwaka kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii.
Alisema kuwa mapato yanakusanywa kwa ufanisi mzuri na kinachokusanywa ndicho kinachotumika na hakuna tatizo la matumizi ndani ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa hivi sasa.