Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima (kulia)akisalimiana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi alipowasili Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
…………………………..
Na Lydia Churi- Mahakama, Musoma
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameiomba Serikali mkoani Mara kuwahamasisha wananchi kujitokeza kutoa ushahidi Mahakamani pale wanapohitajika hatua itakayosaidia kesi kumalizika kwa wakati.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima, Jaji Kiongozi amesema hivi sasa kesi nyingi hazimaliziki kwa wakati kutokana na wadau wa Mahakama kutokukamilisha wajibu wao kwa wakati ikiwemo polisi kutokukamilisha upepelezi wa kesi mapema pamoja na mashahidi kukosekana Mahakamani.
“Hakimu yupo, na ukiangalia jalada utakuta kesi imeahirishwa mara nyingi kutokana na mashahidi kutofika mahakamani”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama kwa upande wake itatoa ushirikiano mkubwa kwa wadau wake pamoja na Serikali ili wananchi wapate haki kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mlundikano wa kesi mahakamani unakwisha.
Aidha, Jaji Kiongozi pia amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Mara kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi ambao hawaridhishwi na huduma zinazotolewa na Mahakama kutumia mifumo ya Mahakama iliyopo ili kufikisha malalamiko yao.
Aliitaja mifumo hiyo kuwa ni pamoja na Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama za Mikoa zinazoongozwa na Wakuu wa Mikoa, Kamati za Maadili za Wilaya zinazoongozwa na Wakuu wa Wilaya pamoja na Kamati ya Maadili ya Majaji.
Jaji Kiongozi pia amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa kuwahimiza wakuu wa wilaya za Mkoa wa Mara kuzisimamia kikamilifu Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama hasa kupitia Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) pamoja na Makatibu Tawala wa Wilaya (DAS).
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Adamu Malima ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mahakama ya Tanzania na kuahidi kuzisimamia kikamilifu Kamati za Maadili. Aliongeza kuwa yote ya dola inalo jukumu la kuwatumikia wananchi na kuwapatia huduma zilizo bora.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama mkoani Mara wakati akihitimisha ziara yake, Jaji Kiongozi amewataka watumishi hao kuikana rushwa na maadili yasiyofaa na badala yake wawe na maadili mema ndani na hata nje ya Mahakama.
Amewapongeza watumishi wasiojishirikisha na vitendo vya rushwa na kuwataka kuwa makini na kujilinda wasije wakaingia kwenye vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili ya utumishi.
Aidha, aliwataka watumishi wa Mahakama kuwakanya na kuwarejesha kwenye mstari watumishi wenzao wanaojishirikisha na vitendo vya rushwa na maadili yasiyofaa badala ya kufurahia pindi wanapopata matatizo.
“Mahakama ni Taasisi kubwa hivyo watumishi wake hawana budi kuwa na upendo kati yao na endapo mtu anakosea aambiwe na kurekebishwa na siyo kusemwa pembeni, tulindane na kupendana sisi kwa sisi”, alisema Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania amemaliza siaza ya siku tano ya kikazi katika Mkoa wa Mara ambapo alikagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime na Musoma Mjini. Jaji Kiongozi pia alikagua jengo jipya la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma lilimalizika hivi karibuni.