Home Uncategorized TMA WATOA UTABIRI WA MVUA MWEZI NOVEMBA HADI APRILI 2019/2020

TMA WATOA UTABIRI WA MVUA MWEZI NOVEMBA HADI APRILI 2019/2020

0

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA Dkt. Agnes Kijazi akizungumza wakati alipotangaza utabiri wa hali ya hewa kuhusu uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka katika makao mkuu ya mamlaka hiyo jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es salaam leo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)Dkt. Agnes Kijazi akisikiliza maelezo ya mmoja wa watabiri wa hali ya hewa alipokuwa akitoa maelezo kuhusu utabiri huo leo katika makao makuu (TMA) jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es salaam kulia ni Dkt. Hamza Kabelwa Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA wa pili kutoka kushoto ni Bw. Samwel Mbuya Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri TMA.

*********************************

MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini(TMA),imetoa utabiri wa muelekeo wa mvua za msimu Novemba hadi Aprili 2019/2020 na kusema kuwa mvua zinazotarajia kunyesha katika maeneo mengi yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinatarajia kuwa za wastani hadi juu ya wastani.

Huku mvua nyingi inatarajia kunyesha katika nusu ya kwanza ya msimu kutokana na uwezekano wa uwepo wa upepo kuvuma kutoka upande wa magharibi.

Akizungumza Dar as Salaam Jana akitoa utabiri wa msimu huo,Mkurugenzi wa TMA,Dkt Agness Kijazi alisema upepo huo unatarajia kubeba unyevunyevu Kutokana misitu ya Kongo kuelekea katika maeneo ya nchi yetu.

Alisema kwa upande wa kipindi cha nusu ya pili cha msimu mvua zinatarajiwa kupungua katika baadhi ya maeneo kutokana na joto la bahari sehemu ya kati ya bahari ya Hindi kuendelea kuongezeka ikilinganishwa na maeneo mengine ya bahari ya Hindi.

“Mvua za msimu ni mahsusi katika maeneo ya magharibu mwa nchi ,kanda ya kati ,nyanda za juu kusini magharibi,kusini mwa nchi,ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro ambapo maeneo haya yanapata msimu mmoja wa mvua ambazo zinaanza mwezi Novemba hadi Aprili ya mwaka unaofuata,” alisema Dkt.Kijazi

Alisema katika mkoa wa ,
Tabora mvua inatarajia kunyesha juu ya wastani hadi wastani huku mkoa wa Kigoma na Katavi inatarajia kunyesha mvua za wastani hadi juu ya wastani na kutarajia kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba 2019katika mkoa wa kigoma na kusambaa Kwa mikoa ya Katavi na Tabora katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba.

“Mvua katika maeneo ya Singida na Dodoma zinatarajia kuanza katika wiki ya Kwanza hadi wiki ya pili ya mwezi Novemba 2019na maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani hadi wastani,” alisema na kuongeza

“Katika mikoa ya Rukwa,Songwe,Mbeya,Iringa,Njombe,Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro mvua zinatarajia kuanza kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2019 na kutarajia kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi,” alisema

Aidha alisema katika mikoa ya Lindi na Mtwara mvua zinatarajia kunyesha kati ya wiki ya kwanza na wiki ya pili ya mwezi Novemba 2019 na zinatarajia kuwa za juu ya wastani hadi wastani.

Dkt.Kijazi alisema kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani.

Alisema migandamizo midogo ya hewa pamoja na vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi inatarajiwa kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo na hivyo kusababisha mvua katika maeneo mengi hapa nchini.

Dkt.Kijazi ametoa ushauri Kwa watumiaji wote wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima,wafugaji,mamlaka za wanyamapori,sekta za maji na afya kuendelea kufuatilia na kutumia ushauri wa kitaalam katika shughuli zao za kila siku.