Home Mchanganyiko Tanzania kupokea watalii zaidi ya 1000 kutoka Israel

Tanzania kupokea watalii zaidi ya 1000 kutoka Israel

0

***********************************

Na Mwandishi wetu,

Tanzania inatarajia kupokea watalii zaidi ya 1000 kutoka nchini Israel ambao
wanakuja nchini kwa ajili ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii mwezi huu
wa Oktoba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe, kundi la kwanza la watalii
hao lililokuwa na zaidi ya watalii 200 wamewasili nchini kuanzia tarehe 05
Oktoba na kundi la pili lenye zaidi ya watalii 520 linatarajiwa kuwasili nchini
tarehe 12 mwezi Oktoba.

Kundi la tatu lenye watalii zaidi ya 200 litawasili nchini tarehe 13 Oktoba kupitia
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Watalii wengine zaidi
wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi huu baada ya makampuni ya uwakala wa
utalii kukamilisha taratibu za safari zao.

“Watalii hao wanatarajiwa kutembelea Visiwa vya Zanzibar, Hifadhi za Taifa za
Serengeti, Tarangire na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Ujio wa watalii hao
unatokana na jitihada za kuitangaza nchi zinazofanywa na Wizara ya Mambo ya
Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania
nchini Israel kwa kushirikiana na wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi”
Taarifa inasomeka.

Aidha, taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki imethibitisha kuwa, Tanzania imejipanga
kuwapokea na kuwatembeza watalii hao katika vivutio vya utalii vilivyoko nchini.

“Serikali inawakaribisha watalii hao kutembelea vivutio hivyo vya utalii ambavyo
nchi imebarikiwa kuwa navyo ili wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza
Tanzania nchini kwao na kwingine watakakokwenda”. Taarifa inasomeka.

Mwezi Aprili 2019, Serikali ilipokea watalii 1,000 kutoka Israel. Aidha, mwezi Mei,
2019 serikali pia ilipokea watalii 330 wakiwemo wafanyabiashara na wawekezaji
kutoka jimbo la Zhejiang, China ambao waliwasili kupitia Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro, KIA. Watalii hao walikuwa ni kundi la kwanza miongoni
mwa watalii 10,000 ambao wanatarajiwa kutembelea Tanzania mwaka huu 2019.