Home Michezo MFUKUZENI ZAHERA KWA SABABU STAHIKI

MFUKUZENI ZAHERA KWA SABABU STAHIKI

0

Na.Imani Kelvin Mbaga,Dar es Salaam

Nazunguka vijiweni na maeneo mahususi ya mijadala ya michezo hasa mpira wa miguu, nakutana na mjadala mkubwa juu ya kiwango na matokeo ya timu ya Yanga, katika michezo ya kitaifa na kimataifa.

Yanga hadi sasa imecheza jumla ya michezo saba ya kimashindano, mitatu kwenye ligi kuu Tanzania na minne kwenye ligi ya mabingwa barani Afrika.

Katika michezo hiyo, Yanga wameshinda miwili, wametoka sare mitatu na kufungwa michezo miwili.

Inafahamika wazi kwamba waalimu wa soka ndiyo “waathirika” wa kwanza wa matokeo ya timu kwakuwa huwa wanawajibika moja kwa moja kwa matokeo ya timu, ndiyo maana upo msemo unaosema “makocha wanaajiriwa ili kufukuzwa”.

Pamoja na yote hayo, wana Yanga wanatakiwa kurudi nyuma na kufanya tathmini ya kinachotokea ili kuchukua hatua sahihi.
Tunafahamu changamoto ya kiuchumi ambayo klabu ilipitia kwa kipindi kirefu hasa msimu uliopita.

Athari za hali mbaya ya kiuchumi zilionekana wazi kiwanjani ambapo Yanga ilipoteza ubingwa kwa mahasimu wao, na pia ikashindwa kushiriki ktk michuano ya kimataifa huku ikishuhudia watani wao wakifika robo fainali ya klabu bingwa Afrika.

Juhudi za wanachama, wapenzi na mashabiki za kuchangia klabu yao ili kufanya usajili wa maana utakaowawezesha kufanya vzr katika michuano wwnayoshiriki.

Tatizo ninaloliona, wapenzi wengi wa Yanga, walitarajia makubwa kwa kipindi kifupi baada ya kufanya usajili. Hakuna anayezingatia juu ya maandalizi ya timu yamekuaje na mabadiliko ya ratiba za shirikisho la soka barani Afrika ambazo kwangu mimi ndiyo sababu halisi za kile ambacho Yanga wanakipitia.

Habari za Yanga kushiriki michuano ya kimataifa zilikuja nje ya mipango ya klabu ya msimu huu, hivyo maandalizi yao yalihitaji kuwa ya muda mfupi kadri iwezekanavyo ili kupata matokeo.

Yanga wameondokewa na wachezaji muhimu “key players” wa msimu uliopita, Ibrahim Ajib, Heritier Makambo, Gadiel Michael ni baadhi ya wachezaji muhimu walioondoka, masuala ya malipo yakawachelewesha Kelvin Yondan, Juma Abdul na Andrew Vincent ambaye hadi sasa hajajiunga na timu hiyo.

Kutoka kwenye kuondokewa na wachezaji muhimu, mgogoro wa kimaslahi, kuunganisha tumu mpya hadi kwenda kucheza na klabu zoefu na ngumu katika michuano ya Afrika panahitaji utimamu wa kimwili na kisaikolojia kwa wachezaji na benchi la ufundi.

Kwa sababu hiyo, Yanga hawakutakiwa kudai makubwa kwa timu yao msimu huu kama wanavyotaka iwe badala yake wanatakiwa kuipa nguvu ili iweze kujijenga na kuwa timu bora hasa msimu unaokuja.

Mapungufu ya Yanga mengi ni ya kiufundi ambayo hayatatuliki kwa muda mfupi, badala yake yanaweza kupata dawa kwa kuondoa shinikizo dhidi ya timu na benchi la ufundi.

Mwisho niseme timu zetu zinahitaji zianze kujipanga kufanya mambo kwa weledi zaidi kuliko kishabiki na shinikizo la utani wa jadi ili kufikia mafanikio makubwa mbeleni.
Mfukuzeni Zahera lakini kwa kuangalia sababu stahiki, msikurupuke