Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC akizungumza na Wanahabari katika ofisi za kituo hicho leo Jijini Dar es Salaam.
***************************
NA EMMANUEL MBATILO.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa wito kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuta adhabu ya kifo kwa wafungwa katika sheria zinazoainisha kosa hilo na kuweka mbadala wa adhabu hiyo ikiwemo kifungo cha maisha au adhabu nyingine isiyohusisha kuua.
Ameyasema hayo leo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Bi.Naemy Sillayo katika ofisi za kituo hicho jijini Dar es Saalam.
Akizungumza katika mkutano huo, Bi.Naemy amesema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwa taifa lililo katika mwelekeo wa kufuta adhabu ya kifo kwani mara ya mwisho adhabu hiyo kutekelezwa ni mwaka 1994, takribani miaka 25 iliyopita.
“LHRC inasisitiza uwepo wa utayari wa kufutwa kwa adhabu hiyo katika sheria zetu na kuwa na adhabu ya kifungo cha maisha kama adhabu mbadala”. Amesema Wakili Bi.Naemy.
Aidha, Bi.Naemy amesema kuwa ibara ya 14 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1997 inalinda haki ya kuishi kwa kila mtu na hata hivyo ibara hii inaathiriwa na sura 16 ya sheria za makosa ya Jinai zinazoweka adhabu ya kifo kwa kosa la uhaini, mauaji na ugaidi.
Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania, 2018 jumla ya watu 480 wapo kwenye orodha ya watu waliohukumiwa adhabu ya kifo wakiwa gerezani kusubiri kunyongwa.