Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo.
Baadhi ya Watumishi wa Umma kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza wakati wa kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo.
Afisa Utumishi Mwandamizi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Elisha Msengi akijibu hoja wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) na watumishi wa Halmashauri ya Meatu kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Wilaya.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza alipowasili katika ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu katika ziara yake ya kikazi ya kuzungumza na watumishi wa Halmashauri hiyo.
…………………………
Na Happiness Shayo- MEATU
Serikali imewataka waajiri nchini kuweka kipaumbele katika programu za mafunzo kwa Watumishi wa Umma ili kuwajengea uwezo kiutendaji kwa kuzingatia Kanuni za Maadili ya kiutendaji.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya hiyo.
“Waajiri hakikisheni mnatoa mafunzo kwa watumishi wenu ili kuendana na kasi ya Sayansi na Teknolojia ikiwa ni pamoja na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Dkt. Mwanjelwa ametoa wito huo baada ya kubaini kuwepo kwa uelewa mdogo wa masuala ya kiutumishi kwa baadhi ya watumishi wa umma wilayani humo.
“Nimegundua bado kuna ombwe la uelewa mdogo wa miiko ya kazi miongoni mwa watumishi wa umma unaosababisha kufanya kazi kwa mazoea, hivyo mafunzo yatawasaidia kuboresha utendaji kazi wao.” Dkt. Mwanjelwa ameongeza.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kuwa na utaratibu wa kujiridhisha kama Waajiri wanawapeleka watumishi kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ili wawe na ufanisi kiutendaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa kufanya ziara wilayani hapo na kuahidi kutekeleza maagizo yote aliyoyatoa.
Dkt. Mwanjelwa amehitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji na watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero za watumishi hao na kuzitatua.