Home Mchanganyiko RUZUKU YA TASAF YABORESHA MAISHA YA WANAKIJIJI WA MKWANDA

RUZUKU YA TASAF YABORESHA MAISHA YA WANAKIJIJI WA MKWANDA

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb)
akizungumza na Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
wa Kijiji cha Mkwanda wilayani Tunduru akiwa katika ziara yake ya
kikazi wilayani humo yenye lengo kukagua utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini mkoani Ruvuma.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mkwanda wilayani Tunduru, Bw. Adam S.
Mboka akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Maskini kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H.
Mkuchika (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya waziri huyo
wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa Mpango wa
Kunusuru Kaya Maskini mkoani Ruvuma.

Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Kijiji cha
Mkwanda wilayani Tunduru, Bi. Aisha Jongo akitoa ushuhuda wa
mafanikio aliyoyapata kupitia TASAF kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt.
(Mst), Mhe. George H. Mkuchika (hayupo pichani) wakati wa ziara ya
kikazi ya waziri huyo wilayani humo yenye lengo kukagua utekelezaji
wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Ruvuma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akisoma
bango linaloutambulisha Mradi wa Bwawa la Samaki unaotekelezwa
na wanufaika 82 wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa kijiji cha
Mkwanda wilayani Tunduru alipoutembelea mradi huo kwa lengo la
kujionea shughuli zinatofanywa na wanufaika hao.

Mradi wa Bwawa la Samaki unaotekelezwa na wanufaika 82 wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Mkwanda
wilayani Tunduru. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H.
Mkuchika (Mb) ametembelea mradi huo.

*************************

Na James K. Mwanamyoto, Tunduru

Tarehe 9 Oktoba, 2019

Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa kijiji cha Mkwanda
wilayani Tunduru wamekiri kuboresha maisha yao baada ya kupokea ruzuku
kupitia Mpango huo unaotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuzinusuru kaya
maskini ambazo zinahitaji msaada wa kujikwamua kiuchumi.

Baadhi ya wanufaika wa Mpango huo wameeleza hayo wakati wa mkutano wa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) na wanufaika hao, uliofanyika
katika kijiji hicho wenye lengo la kubaini mafanikio na changamoto za Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini.

Akitoa shuhuda wakati wa mkutano, mmoja wa wanufaika Bi. Aisha Jongo
amesema TASAF imemuwezesha kuboresha makazi yake kwa kuezeka bati
kwenye nyumba yake na kujenga nyumba nyingine ya bati.

“Awali nilikuwa nikiishi kwenye nyumba ya nyasi, nilipoanza kupokea ruzuku
nilianza kununua bati moja moja mpaka zikatimia ishirini na kupaua nyumba
yangu na kafanikiwa kujenga nyumba nyingine ya bati”, Bi. Jongo amefafanua.

Bi. Jongo ameongeza kuwa, kupitia TASAF ameweza kununua sola
inayomuwezesha kupata umeme wa uhakika, hivyo ameachana rasmi na
matumizi ya kibatari.

Naye, Bw. Issa Shaban Mfaume amesema yeye na wazazi wake wamenufaika
na Mpango kiasi cha kuweza kujenga nyumba wanayoishi sasa, hivyo TASAF
imekuwa na manufaa kwani wanaishi kwenye nyumba iliyoezekwa kwa bati.

Bw. Mfaume amemthibitishia Mhe. Mkuchika kuwa, awamu ya pili ya Mpango
imemuwezesha kuwa na bwawa la kufugia samaki linalomuingizia kipato na
hatimaye kuendesha maisha yake na ya familia yake vizuri.

“Hamasa na elimu ya kuanzisha bwawa langu la samaki nimeipata kupitia Mradi
wa Bwawa la Samaki la kijiji cha Mkwanda ambalo ni la walengwa wa Mpango
wa Kunusuru Kaya Maskini”, amesisitiza Bw. Mfaume.

Akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) kuzungumza na
wanufaika hao, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mhe. Julius Mtatiro amewaasa
wanufaika hao kubuni miradi mbalimbali itakayowawezesha kutumia vema
ruzuku wanayoipata kuondokana na umaskini.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb)
amewapongeza wanufaika hao kwa kutumia vizuri ruzuku kuboresha maisha
yao, na kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ruzuku kupitia Mpango huo ili
kutekeleza azma ya kuzinusuru kaya maskini.

Mhe. Mkuchika amewatembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini wa kijiji cha Mkwanda wilayani Tunduru ikiwa ni sehemu ya ziara yake
ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani
Ruvuma.