Mwanasheria na Afisa Mlinda Mlaji wa Tume ya Ushindani (FCC) Exavery Ngelezya (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu elimu ya utambuzi wa bidhaa bora na bandia iliyotolewa kwa wananchi katika maonesho ya pili ya viwanda vidogo (SIDO) Kitaifa 2019 yanayoendelea Uwanja wa Bombadia Mkoani Singida. Kulia ni Afisa Uhusiano na Mawasiliano ya Umma, Adefrida Ilomo.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano ya Umma wa FCC, Adefrida Ilomo akizungumza na waandishi wa habari.
Na Dotto Mwaibale, Singida
TUME ya Ushindani (FCC) imetoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali katika maonesho ya pili ya viwanda vidogo (SIDO) Kitaifa 2019 mkoani Singida kuhusu bidhaa bandia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika maonesho hayo Afisa Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa tume hiyo Adefrida Ilomo alisema tume hiyo imetoa elimu kwa wananchi kuhusiana na utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
“Tumekusudia kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda letu inayohusu masuala ya ushindani, utetezi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia” alisema Ilomo.
Ilomo alisema tume hiyo imeanza kutoa elimu ya wajibu wa wazalishaji na wajasiriamali katika kusajili nembo zao ili waweze kulindwa na sheria ya alama za bidhaa dhidi ya wazalishaji wanaoiga bidhaa zao kwa nia ya kudanganya au kutapeli.
Alitaja wajibu mwingine wa wazalishaji au wajasiriamali ni kuhakikisha wanaonesha taarifa zote muhimu katika vifungashio kwa mujibu wa sheria au alama za bidhaa ya 1963 na sheria ya ushindani ya mwaka 2003 na kuwa wajibu wa wafanyabiashara na watoa huduma ni kuwasilisha taarifa zao kwa ajili ya mapitio ya mikataba yote ya mlaji.
Mwanasheria na Afisa Mlinda Mlaji wa FCC Exavery Ngelezya alitoa wito kwa wananchi kutambua bidhaa bora na kuzibaini zile za bandia ili kuepuka madhara yatokanayo na bidhaa hizo bandia.
Kwa upande wa wajasiriamali wametakiwa kuhakikisha kutomlisha mlaji bidhaa zisizo na ubora hivyo ni vyema kupitia taratibu zote kabla ya kupeleka bidhaa zao sokoni