Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(kulia) akikagua matofali ya kuchoma katika mradi wa ufyatuaji tofali za kuchoma katika gereza la wilaya ya Mbozi alipotembelea hivi karibuni katika ziara yake ya kikazi Mkoani Songwe.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akikagua moja ya tanulu la matofali ya kuchoma katika mradi wa ufyatuaji tofali za kuchoma katika Kambi ya Mkwajuni , Wilayani Songwe, leo Oktoba 8, 2019 alipotembelea katika ziara yake ya kikazi Mkoani Songwe.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike akiwasili jana Oktoba 7, 2019 katika ziara yake ya kikazi Gereza Ngwala.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Samwel Opulukwa(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike(wa pili toka kulia) alipotembelea Ofisi za Mkuu wa Wilaya hiyo leo Oktoba 8, 2019. Kulia ni Mkuu wa Magereza Mkoani Songwe, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Lyazeck Mwaseba(Picha na Jeshi la Magereza.
……………………..
Na Mwandishi wetu, Songwe;
KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amewataka Wakuu wa magereza Tanzania Bara kuhakikisha kuwa wanatekeleza ipasavyo agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu ujenzi wa nyumba za makazi ya askari wa jeshi hilo kote nchini kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa waliopo magerezani.
Akizungumza Mkoani Songwe mara baada ya kukagua miradi ya ufyatuaji wa matofali ya kuchoma na ujenzi wa nyumba za maafisa na askari katika magereza ya Ileje, Mbozi, Ngwala na Kambi ya Mkwajuni iliyopo Mkoani Songwe, Kamishna Jenerali Kasike amesema ujenzi wa makazi za askari unaoendelea katika vituo mbalimbali nchini ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli katika kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi wa Jeshi hilo.
“Mkakati wa utatuaji wa changamoto ya uhaba wa nyumba za Maafisa na askari lazima utiliwe mkazo na kupewa kipaumbele katika kuwatumia wafungwa waliopo magerezani katika suala la ujenzi sambambamba na uzalishaji wa chakula chakutosha ili kuipunguzia Serikali gharama za kuwahudumia wahalifu wote walipo magerezani, ” alisema Kamishna Jenerali Kasike.
Katika hatua nyingine, Kamishna Jenerali Kasike ameupongeza Uongozi wa Wilaya ya Songwe kwa kuanzisha ujenzi wa Gereza jipya katika mji wa Mkwajuni ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Songwe.
Kamishna Jenerali Kasike amesema uwepo wa gereza hilo katika wilaya ya Songwe utasaidia katika kumaliza tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye gereza la wilaya ya Mbozi.
“Kutokuwepo kwa magereza ya wilaya kunasababisha msongamano wa wafungwa na mahabusu katika magereza ya jirani, pamoja na kuchelewesha upatikanaji wa haki hivyo nimpongeze sana Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Mhe. Samwel Opulukwa pamoja na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwa kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa Gereza hili kimsingi utatatua tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza Mbozi,” amesema Jenerali Kasike.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Songwe. Mhe. Samwel Opulukwa ameshukru ujio wa Kamishna Jenerali katika ziara yake ya kikazi katika Gereza la Ngwala pamoja na Kambi ya Mkwajuni ili kujionea hali halisi ya Uendeshaji wa Jeshi hilo, Wilayani Songwe.
“Kamishna Jenerali nikuhakikishie tu kuwa Uongozi wa wilaya utashirikiana na Jeshi la Magereza katika kuhakikisha kuwa tunakamilisha ujenzi wa gereza hili jipya la Mkwajuni ili kusaidia kuondoa usumbufu wa wahalifu kwenda gereza la wilaya ya mbozi,” Alisistiza Mhe. Opulukwa.
Kwa sasa, wakazi wa wilaya hiyo ya Songwe ambao wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali au waliohukumiwa vifungo hupelekwa katika Gereza la wilaya ya Mbozi kitendo ambacho kinawanyima wafungwa na mahabusu fursa ya kuonana na ndugu au mawakili wao kutokana na umbali uliopo ambapo kutokana na juhudi za Mkuu wa Wilaya hiyo tayari Bweni moja la Wafungwa lenye uwezo wa kuhifadhi waha;lifu 150 limekamilika pamoja na Ofisi ya Utawala na ujenzi wa Ukuta wa gereza unaendelea katika Kambi hiyo ya Mkwajuni.