NJOMBE
Baada ya Serikali kuutangazia umma muda wa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura , hatimae chama cha mapinduzi kupitia kwa makamu mwenyekiti wake bara Philip Mangula kimezindua zoezi hilo katika kijiji cha Kinenulo kilichopo kata ya Imalinyi wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.
Siku Chache zilizopita waziri wa ofisi ya rais TAMISEMI Suleman Jafo alitangaza octoba 8 hadi 14 kuanza kufanyika zoezi la uandikishaji wa wapiga kote nchini ikiwa ni hatua ya maandalizi ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa wenye lengo la kuwapata wenyeviti na wajumbe wa serikali unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu.
Awali akiungumza na wakazi wa kijiji cha Kinenulo mara baada ya kufanya uzinduzi kwa kuwa mtu wa kwanza kujiandikisha makamu mwenyekiti wa chama cha mapinduzi bara Philip Mangula amewataka wananchi wenye sifa ya kupiga kura kujiandikisha ili kukidhi vigezo vya kushiriki katika uchaguzi huo ambao utawafanya kupata viongozi wapya wa serikali za mitaa huku akiwataka kuchagua viongozi wenye uchungu na taifa letu
Akifafanua kuhusu utaratibu uliyowekwa na serikali kuhusu uendeshaji wa zoezi hilo Comrade Ally Kassinge ambaye ni mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe amesema vituo 525 vimetengwa huku akiwatoa hofu wananchi kuhusu suala la usalama kipindi cha uandikishaji na uchaguzi.
Nao baadhi ya wakazi waliojitokeza kujiandikisha akiwemo Fanuel Chengula na Anna Mtonya wanasema wamehamasika kushiriki katika chaguzi kwani wamedhamilia kupata viongozi bora wakuwaongoza miaka mitano ijayo.
Wakazi hao wamesema picha ya awali inaonyesha mwamko umeongezeka jambo ambalo litawafanya kupata viongozi bora