Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi
(kushoto) akiagana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika na kupokewa na Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza
(katikati) wakati akiwasili wilayani Bunda kuanza ziara ya kikazi katika
mkoa wa Mara.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Bunda wakimsikiliza Jaji Kiongozi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (hayupo
pichani) alipokuwa akizungumza nao.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi
(kushoto) akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Bunda Bibi Lydia Bupilipili
alipowasili ofisini kwa Mkuu huyo wa wilaya wakati akianza ziara ya
kikazi katika mkoa wa Mara.
*****************************
Na Lydia Churi-Mahakama, Bunda
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema
Mahakama inakusudia kupunguza kuwatumia wazee washauri wa Mahakama
katika kuamua mashauri Mahakamani na itabaki ikiwatumia katika mashauri
ambayo yataonekana yana ulazima wa kuwatumia wazee hao.
Akizungumza wilayani Bunda ambapo ameanza ziara ya kikazi kukagua shughuli
za Mahakama katika Mkoa wa Mara, Jaji Kiongozi amesema wazee hao
watatumiwa na Mahakama kwenye mashauri ambayo yatakuwa na ulazima wa
kuwatumia lakini yale ambayo siyo lazima, wazee hao wataacha kutumiwa.
Jaji Kiongozi amesema baadhi ya wazee washauri wa Mahakama hujishirikisha na
vitendo vya rushwa na wakati mwingine huwatisha Mahakimu wanapokuwa
wakitekeleza wajibu wao.
Alisema matumizi ya wazee washauri wa Mahakama wakati mwingine
husababisha mashauri kuchelewa kumalizika kutokana na kuchelewa kwao kufika
Mahakamani na kusababisha mashauri kutokusikilizwa kwa wakati.
Akizungumza kuhusu rushwa, Mhe. Dkt, Feleshi alisema Mahakama kama Taasisi
haijishirikishi na vitendo vya rushwa bali vitendo hivyo hufanywa na baadhi ya
watumishi wasio waaminifu ndani ya Mahakama.
“Tuachane na maneno mepesi mepesi kuhusu rushwa kwa kuwa taarifa zipo,
pelekeni Takukuru, hakuna anayemlinda mtu”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama itashirikiana na Serikali katika kupambanana na rushwa na
hivvo aliwataka wananchi wenye taarifa juu ya vitendo hivyo kuwasilisha kwenye
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa –Takukuru.
Aidha, Mhe. Dkt. Feleshi amesema Mahakama na Serikali katika wilaya ya Bunda
wanapaswa kushirikiana katika kutatua changamoto nyingine mbalimbali za
wananchi kwa kuwa wote wanamtumikia mwananchi.
Akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Bunda, Jaji Kiongozi
amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kubeba matarajio ya
Taasisi kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aliwataka Mahakimu kumalizika mashauri kwa wakati, pamoja na kutoa nakala za
hukumu na mienendo ya mashauri ndani ya muda uliopangwa ambao kwa nakala
za hukumu ni siku 21 tangu kumalizika kwa shauri na mienendo ya shauri
hutolewa ndani ya siku 30.
Aidha, aliwataka watumishi hao kujenga tabia ya kutafuta na kufahamu taarifa
mbalimbali za Mahakama kupitia Tovuti pamoja na Blog ya Mahakama ya
Tanzania.
Naye Mkuu wa wilaya ya Bunda Bibi Lydia Bupilipili amewashauri Watumishi wa
Mahakama kujenga mazingira yatakayowafanya wananchi kuendelea kuiamini
Mahakama ya Tanzania kwa kutoa huduma zilizo bora kwa wananchi.
Alisema Serikali pamoja na Mahakama wilayani Bunda wanashirikiana katika
kutatua baadhi ya changamoto za Mahakama huku akitoa wito kwa Mahakimu
kutumia njia ya usuluhishi katika kutatua baadhi ya migogoro miongoni mwa
wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya pia aliishauri Mahakama ya Tanzania kujikita katika kutoa
elimu kwa wananchi hasa kwenye maeneo yenye changamoto zaidi wakati wa
maadhimisho ya wiki ya sheria ambayo hufanyika kila mwaka nchini.
Alisema wananchi hawana budi kufahamu taratibu mbalimbali za Mahakma
hususan zile za ufunguaji wa mashauri Mahakamani.
Jaji Kiongozi ameanza ziara ya kikazi ya siku tano Mahakama Kuu ya Tanzania
kanda ya Musoma ambapo atakagua shughuli mbalimbali za Mahakama katika
wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime pamoja na Musoma.