NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla Mabodi, akifungua Mafunzo Elekezi kwa Makatibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja wa ngazi za Matawi hadi Mkoa yaliyofanyika Chuo Cha Utawala wa Umma Tunguu Zanzibar.
WASHIRIKI wa Mafunzo Elekezi ya kuwajengea uwezo Makatibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja wakisikiliza Hotuba ya Mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mafunzo hayo.
Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, ambaye pia ni Katibu Katibu wa CCM Mkoa huo Suleiman Mzee Suleiman, akitoa ufafanuzi juu ya Mafunzo hayo elekezi kwa Makatibu wa CCM ngazi za Matawi hadi Mkoa, yaliyofanyika Chuo Cha Utawala wa Umma Tunguu Zanzibar.
………………………………………
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, amewata Makatibu wa Chama hicho kubuni masuala mbali mbali ya kiutendaji yatakayoongeza ufanisi katika Shughuli za Chama na Jumuiya zake.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mafunzo elekezi kwa Makatibu wa CCM ngazi za Matawi hadi Mkoa katika Mkoa wa Kusini Zanzibar, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utawala wa Umma Tunguu, Zanzibar.
Dk.Mabodi alisema mafunzo hayo yamefanyika katika wakati mzuri wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Dola wa Mwaka 2020,hivyo Watendaji hao wanatakiwa kujifunza kwa bidii ili watekeleze kwa ufanisi shughuli za Chama.
Naibu Katibu Mkuu huyo, aliwambia Makatibu hao kuwa wanatakiwa kufanya kazi zao kwa mujibu wa miongozo ya CCM na kuepuka kufanya kazi za Wanasiasa ikiwa wao wanakabiliwa na majukumu ya kiutendaji.
Pamoja na hayo alisisitiza kila Mtendaji kuendeleza kwa vitendo dhana ya kushuka kwa wananchi wa ngazi mbali mbali kwa lengo la kuratibu changamoto zao ili zifanyiwe kazi na Mamlaka husika.
Katika maelezo yake Dk.Mabodi aliwasihi Makada Wasomi Nchini kuhakikisha elimu waliyonayo wanawafundisha Wanachama wengine ili Chama kiwe imara katika masuala ya Uongozi,Utawala,Uchumi na Kijamii.
Aidha Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi, aliwapongeza Viongozi mbali mbali wa Mkoa huo kwa juhudi zao za kulinda heshima ya Mkoa huo kwa vitendo na ukaendelea kuwa ngome ya CCM Kisiasa.
“Washiriki nyote wa mafunzo nakutakeni baada ya kurudi katika maeneo yenu ya kiutendaji mlete mabadiliko chanya yatakayoongeza ufanisi ndani ya Chama Cha Mapinduzi”, alisema Dk.Mabodi na kuongeza kuwa wanatakiwa kufanya kazi kwa vitendo na kufkiria kimkakati namna ya kufanikisha majukumu yao.
Kupitia ufunguzi wa mafunzo hayo Dk.Mabodi, aliwakumbusha Watendaji kuepuka vitendo vya rushwa ndani ya Chama kwani vinasababisha madhara ya kupatikana kwa viongozi wasiokuwa waadilifu.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja ambaye pia ni Kimu Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Suleiman Mzee Suleiman alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wa kiutendaji makatibu hao ili wafanye kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Alisema Mkoa huo licha ya kuwa ni ngome ya CCM bado baadhi ya Makatibu wake walikuwa na changamoto ya ukosefu wa uwezo wa kuandaa mitahsari na taarifa mbali mbali za Chama.
Akisoma risala Katibu wa CCM Jimbo la Tunguu Sharifa Maabadi, alisema mafunzo yatatolewa kwa siku Sita na yatawashirikisha Makatibu 120 kuanzia ngazi za wadi hadi Mkoa.
Alisema kupitia mafunzo hayo Makatibu watafundishwa masuala ya Uongozi,Uzalendo,itifaki kwa Viongozi,utunzaji wa habari na kumbukumbu na mbinu za kuzungumza na kuwashawishi watu kuendelea kujiunga na CCM.
Aidha alitoa rai kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu kwani yatawasaidia Viongozi na Watendaji wa CCM katika Mkoa huo kuwa na Weledi na mbinu mbali mbali za kufanya kazi za Chama Cha Mapinduzi kwa mujibu wa maelekezo ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017.