Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Emanuel Chibago akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Kongamano kubwa la kimataifa ambalo huandaliwa na kanisa la Tanzania Fellowship of Churches, lenye lengo la kufanya tathmini ya utendaji wa makanisa yote ya nje na ndani ya nchi, lililofanyika kwa wiki nzima jijini Dodoma.
Askofu na mlezi wa Makanisa ya Tanzania Fellowship of Churches, Godfrey Malasi, akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Kongamano kubwa la kimataifa ambalo huandaliwa na kanisa la Tanzania Fellowship Churches, lenye lengo la kufanya tathmini ya utendaji wa makanisa yote ya nje na ndani ya nchi, lililofanyika kwa wiki nzima jijini Dodoma.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Emanuel Chibago (wapili kulia) akisalimiana na wachungaji wa Makanisa ya Tanzania Fellowship of Churches, baada ya kuwasili Kanisani hapo kufunga Kongamano kubwa la kimataifa ambalo huandaliwa na kanisa hilo lenye lengo la kufanya tathmini ya utendaji wa makanisa yote ya Tanzania Fellowship Churches ya nje na ndani ya nchi, lililofanyika kwa wiki nzima jijini Dodoma.
Muonekano jengo la Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches la Dodoma ambalo linaendelea na ujenzi ambalo sasa litakuwa ndio makao makuu ya makanisa hayo.
……………….
Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.
Taasisi za kidini zimetakiwa kutengeneza utaratibu wa kuwakusanya watoto wanaozulura ovyo mitaani hasa maeneo ya mijini wasiokuwa na walevi kuwasaidia, ikiwamo kuwaandalia vituo maalumu vya kuwalelea watoto hao na kuwapa mafundisho ya kidini sambamba na kuwapa mafunzo mbalimbali.
Wito huo umetolewa Jijini Dodoma na Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Emanuel Chibago, alipokuwa akimuwakilisha Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, wakati wa kufunga Kongamano kubwa la Kimataifa linaloyakutanisha Makanisa yote ya Tanzania Fellowship of Churches kwa pamoja na kutathmini utendaji wao kwa mwaka husika.
Naibu Meya Chibado, amesema taasisi za kidini zina nafsi kubwa ya kuweza kuwashawishi na kuwakusanya watoto wa mitaani na vijana wanaotumia madawa ya kulevya na kuwawekea utaratibu wa kuwapa mafundisho ya kidini yatakayo wawezesha kuachana na tabia hizo ili kuokoa kizazi kijacho.
“Niwaombe viongozi wa dini muweke utaratibu wa kuwakusanya vijana wanaozurula ovyo mitaani wote tunaona watoto wetu wanazurula ovyo na kuvuta gundi na madawa ya kulevya wakusanyeni na kuwapa mafundisho ya kidini na mafunzo mbalimbali” amesema Chibago.
Pia amewataka viongozi wa dini waanzishe utaratibu wa kutoa elimu ya kutunza fedha na kujiwekea hazina na akiba ikiwamo kuwahamasisha kutokuwa na vikundi vingi vya akiba na kukopa, bali waelimishwe namna bora ya kutunza akiba.
Pia amewapongeza viongozi na waumini wa Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches, upande wa Dodoma kwa kupisha ujenzi wa kitega uchumi cha halmashauri ya Jiji la Dodoma, ambapo kabla ya kuanza ujenzi wa kitega uchumi hicho, ndipo walikuwa wakiabudia, lakini walikubali kuondoka na kuhamia sehemu nyingine kupisha ujenzi huo.
Kwa upande wake Askofu na Mwangalizi wa Makanisa ya Tanzania Fellowship of Churches hapa nchini Godfrey Malasi, amesema makanisa hayo yanautaratibu wa kukutana kila mwaka kwa pamoja na kufanya tathmini ya utendaji kazi wao kwa mwaka husika ni namna gani wameweza kuifikia jamii katika maeneo husika.
Amesema malengo yao ni kuifikia jamii kwa ukubwa wake na ndio maana wanautaratibu wa ibada za nyumba kwa nyumba lengo likiwa ni kuhakikisha wanaifikia jamii kwa wingi na kuwapa neno la Mungu, pia wanautaratibu wa kutembelea jamii na kutoa misaada kama kanisa, kama kusaidia watoto yatima, watoto wasiojiweza, wajane, wagonjwa.
Pia katika jamii wanautaratibu wa kutembelea na kukarabati miondombinu ya Shule, vituo vya Afya na vituo vya polisi yote hayo ni kuhakikisha wanarudisha fadhila kwa jamii, sambamba na kwenda kuwatembelea wafungwa magerezani na kuwapa moyo.
“Makanisa yetu yanautaratibu wa kukutana kila mwaka kuangalia utekelezaji wa majukumu tuliyojiwekea kufanya kwa jamii na kuangalia ni wapi tumefikia na kiasi gani tumeifika jamii katika kupeleka injili, na tunautaratibu wa ibada za nyumba kwa nyumba” amesema Askofu Malasi.
Kuhusu kuanzisha vituo vya kulelea watoto wa mitaani amesema tayari kanisa hilo lilishaweka utaratibu wa kuanza kujenga vituo kama hivyo na wapo katika hatua za mwisho kukamilisha na kuanzisha utaratibu huo, na kila kanisa limepewa utaratibu wa namna ya kuanza kutekeleza hayo.
“Bahati nzuri hata kabla ya Naibu Meya kuongelea hayo tayari sisi kama kanisa tulishawahi kuwaza kuanzisha vituo hivyo, na sasa tutaweka mkazo zaidi, mfano kama Afrika kusini tayari tulishaanzisha na vijana wengi waliokuwa wakitumia madawa ya kulevya sasa ni waumini wazuri makanisani” amesema Askofu Malasi.