Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare akikagua moja ya jengo katika shule ya sekondari Morogoro, katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa shue ya Sekondari Morogoro na Shule ya Sekondari Mji mpya zote zilizopo Manispaa ya Morogoro, wa kwanza kulia Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi Regina Chonjo.
Baadhi ya majengo katika Shule ya Sekondari ya Mji Mpya Manispaa ya Morogoro yaliyojengwa kwa fedha ya serikali
…………………………………..
Na, farida saidy – Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo kwa Usimamizi mzuri wa Ujenzi wa Majengo ya Shule za Sekoondari Morogoro na shule ya sekondari Mji Mpya zilizopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Sanare ametoa pongezi hizo Oktoba 3, mwaka huu alipotembelea Shule ya Sekondari ya Morogoro ambayo iko katika hatua za mwisho za ukarabati wa majengo yake na shule ya Sekondari ya Mji Mpya ambayo nayo ujenzi wake upo hatua za mwisho baada ya majengo yake ya awali kubomolewa ili kupisha Ujenzi wa mradi wa Reli ya mwendokasi (SGR) .
Akiwa katika shule ya sekondari Morogoro, Mhe. Sanare amesema Serikali imetoa zaidi ya shilingi billioni moja kwa ajili ya ujenzi huo hivyo ilikuwa ni wajibu wake kukagua namna ya fedha za Serikali zilivyyotumika katika ujenzi huo.
“Serikali imeleta hapa kwenye shule hii zaidi ya shilingi billion moja, hivyo ni jukumu letu kukagua namna fedha ya Serikali ilivyotumika, nashukuru Mungu kazi imekwenda vizuri, nichukue nafasi hii kuipongeza kamati ya shule iliyosimamia ujenzi huu lakini pia nikupongeze Mhe. Mkuu wa Wilaya kwa kazi nzuri ya kusimamia kazi hii,” alisema Sanare.
Aidha, Sanare amemtaka Mkandarasi anaefanya kazi ya ukarabati wa shule hiyo kuhakikisha anakamilisha ujenzi katika muda wa siku kumi alizoongezewa kwa kuwa alipaswa kukamilisha ujenzi huo Septemba 26 mwaka huu.
Amesema anaamini ifikapo tarehe 10 Oktoba mwaka huu atakabidhiwa majengo hayo hivyo ni wajibu wao Wakandarasi wa ujenzi miradi hiyo kuhakikisha wanatumia siku zilizobaki kufanyakazi kwa bidii ili kukabidhi majengo hayo.
Sambamba na hayo Mhe. Sanare amewataka wanafunzi wa shule hiyo kusoma kwa bidii ili kupandisha ufaulu wa shule yao kwa kuwa Serikali imeboresha miundombinu hivyo hakuna sababu ya kutofanya vizuri kwenye mitihani yao.
Ukarabati wa Shule ya sekondari Morogoro iliyoanzishwa mwaka 1954 umegharimu zaidi ya billion 1.04 ukihusisha madarasa 29 majengo kwa ajiliya maabara 4, Ofisi za walimu 17, Jiko, mabweni 8, Ukumbi wa Mikutano, Matundu ya vyoo 85, Mabafu 24, Mfumo wa Maji, Mfumo wa Umeme na nyumba za walimu 12.
Akiwa katika shuleya Sekondari ya Mji Mpya alipokea taarifa ya ujenzi kutoka kwa Mkuu wa shule hiyo Zakayo John na kuelezwa kuwa ujenzi huo unapaswa kukamilika Octoba 25 mwaka huu kwa sasa ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia 88 jambo ambalo alipongeza kwa kasi ya ujenzi na kazinzuri iliyofanyika.
Hata hivyo Mhe. Sanare amemuagiza Mkuu wa Shule hiyo kuishi shuleni hapo punde tu ujenzi wa nyumba mpya ya walimu utakapokamilika badala ya kuishi mbali ya eneo la shule na vinginevyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Regina Chonjo amemshauri Mkuu wa shule ya Mji Mpya kuwa endapo fedha zitabaki kwenye ujenzi wa shule ya mji mpya fedha hizo zitumike kukarabati baadhi ya miundombinu ya Shule ya sekondari Tushikamane ambayo walikuwa wakitumia kwa muda kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa shule yao ya Mji Mpya.
Amesema hali si nzuri katika shule hiyo hasa baada ya kutumiwa na wanafunzi wa shule mbili wakati miundombinu yake ilijengwa kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa shule moja pekee.
Ujenzi wa shule ya Sekondari ya Mji Mpya Umegharimu zaidi ya shilingi billion Moja na nusu ambapo tayari wanafunzi wa shule hiyo wamesharejeshwa katika majengo yao kwa ajili ya kuendelea na masomo wakati baadhi ya majengo yakiendelea kufanyiwa umaliziaji kwenye baadhi ya maeneo.