********************
NJOMBE
Aliyekuwa mwenyekiti na mwanasheria mkuu wa Chadema mkoa wa Njombe Ewdin Enos Swale amerudisha kadi ya chama chake cha awali na kujiunga na chama cha mapinduzi hii leo octoba 6 tukio ambalo limefanyika katika ofisi za CCM wilayani Njombe.
Awali akizungumza mara baada ya kupokelewa na mamia ya wanachama wa chama cha mapinduzi mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa jukwaani amesema amelazimika kurejesha kadi ya chadema kwasababu ya utendaji uliyotukuka wa serikali iliyopo madarakani ambayo kwa kipindi cha miaka minne imebadili kabisa taswila ya mkoa wa Njombe .
Amesema litakuwa jambo la kushangaza kuendelea kumpinga rais Magufuli ambaye amefanikiwa kutekeleza miradi ya mabilioni ya fedha mkoani humo ambapo ameutaja ujenzi unaoendelea wa mradi wa soko lenye hadhi ya kimataifa lililogharimu zaidi ya bil 9, mradi wa kituo cha mabasi wenye thamani ya bil 9.6 huku miradi mingine ambayo ameitaja ya ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete kwa kiwango cha lami , Barabara ya Njombe Ludewa.
Aidha mwanasiasa huyo mashuhuli amesema kitendo cha kutekeleza ujenzi wa hospitali tatu za wilaya, vituo vya afya na Zahanati katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo zimeua kabisa agenda za upinzani ambazo zilikuwa na mashiko kwa wananchi na kuvifanya vyama vya upinzani kupanda nazo majukwani kama agenda zao kuu.
Mara baada ya kupokelewa wakili Swale anatoa rai kwa watanzania kuendelea kumuunga mkoano rais badala ya kumkejeli na kudai kwamba licha ya kuwa mpinzani mkubwa wa mbunge wa jimbo la Lupembe Joram Hongoli katika uchaguzi mkuu wa 2015 ataungana nae sasa katika kupigania maendeleo ya wana Lupembe ambao wamekuwa wakiathiriwa na migogoro ya wao kwa wao ukiwemo wa mmiliki wa kiwanda cha Chai Lupembe .
Kurejea CCM kwa mwasiasa huyo kumemsukuma pia mtoto wa mwanasiasa nguli wa chama cha mapinduzi Msafiri Mpollo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa BAVICHA jimbo la Lupembe ambaye anasema hawezi kuendelea kusalia chama cha demokrasia na maendeleo kwa kuwa atajikuta katika wakati mgumu na huzuni kubwa katika uchaguzi wa 2020 baada wa wagombea wa upinzani watakapo poteza nafasi nyingi watakazo wania.
Mpollo ambaye licha ya kujihusisha na masuala ya siasa lakini pia ni mtumishi wa umma katika shirika la mawasiliano ya simu TTCL anasema kuwa jambo kubwa lililomsukuma kumfuata mwenyekiti wake kujiunga na chama cha mapinduzi ni kitendo cha rasi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma ,ujenzi wa miradi mikubwa ya barabara pamoja na maboresho makubwa ya sekta ya afya.
Akitoa kauli ya chama mara baada ya mapokezi mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Njombe Edward Mgaya amesema uamuzi waliofanya wanasiasa hao wenye ushawishi mkubwa kwa wananchi umekuwa wa busara kubwa na kuwataka kwenda kushirikiana na mbunge wao kupigania maendeleo ya wanalupembe.
“Lupembe ilikuwa na uchumi mkubwa kabla na baada ya uhuru na kwamba kurejea kwa wanasiasa hao chama cha mapinduzi kukasaidie kurejesha tena uchumi wa Lupembe kwenye ramani kama ilivyokuwa awali” alisema Mgaya.