Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Watendaji wa
Mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi kilichofanyika jijini
Mwanza.
Baadhi ya Watendaji kutoka Mkoa wa Mwanza wakimsikiliza Naibu Waziri,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza
wakati wa kikao kazi kilichofanyika jijini Mwanza.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji akijibu hoja
wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb),
Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma na Watendaji wa Mkoa wa
Mwanza kilichofanyika jijini Mwanza.Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (kulia) akiteta jambo na Kamishna
wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe.John Haule wakati wa kikao kazi kati
yake na Watendaji wa Mkoa wa Mwanza kilichofanyika jijini Mwanza.
Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Bw. Said Raphael Kitinga.
*********************************
Na Happiness Shayo, Mwanza
Serikali imewataka watendaji katika taasisi za umma nchini
kutenda haki wanapowahudumia watumishi wa umma ili
kupunguza mlundikano wa rufaa na malalamiko ya watumishi wa
umma yanayowasilishwa Tume ya Utumishi wa Umma dhidi ya
waajiri.
Wito huo umetolewa jijini Mwanza na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt.
Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa kikao kazi chake na Watendaji
wa Serikali mkoani Mwanza kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu
wa Mkoa wa Mwanza.
“Serikali inaamini katika haki na Rais wetu Dkt. John Pombe
Magufuli anataka haki itendeke hususani kwa wanyonge, hivyo
mtendaji yeyote atakaebainika kumuonea mtumishi kwa kumnyima
stahiki yake ni wazi kuwa serikali itamchukulia hatua za
kinidhamu” Dkt. Mwanjelwa amesema.
Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa, Tume ya Utumishi wa Umma
imekuwa ikipokea malalamiko mengidhidi ya watendaji kuwaonea
watumishi wa umma na kuwataka watendaji hao kuwajibika
ipasavyo katika nafasi zao ili kuepukana na malalamiko yasiyo ya
lazima.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa amewaasa watendaji haokutumia muda
wao kuwaelimisha watumishi kuhusu Kanuni, Sheria,
Taratibu,Nyaraka na miongozo ya kiutumishi iliyopo ili watumishi
wapate uelewa wa kutosha kuhusiana na stahiki za kiutumishi
wanazostahili kupata.
“Mtumishi anapokuja ofisini kwako tumia muda wako
kumuelewesha mtumishi huyo juu ya suala lake, kwa sababu ni
sehemu yako ya kazi” Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya watumishi kutobadilishiwa
kazi(recategorization) baada ya kujiendeleza, Katibu wa Tume ya
Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji amewataka Watendaji
hao kuwashauri watumishi walio chini yao kujiendeleza kitaaluma
katika kada zao walizopatia ajira(first appointment).
Bw. Muhoji ametoa wito kwa waajiri nchinikuwaingiza watumishi
katika mpango wa mafunzo na kuwataka kuwapa ushirikiano wa
kutosha watumishi wanaotaka kujiendeleza wenyewe kupitia
vyanzo vyao vya mapato, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa
wametoa fursa kwa watumishi hao kujijengea uwezo kiutendaji”
Bw. Muhoji amesema.
Naye, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela, Bw.Said Raphael
Kitinga akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho,
ameishukuru serikali kwa elimu ya masuala ya kiutumishi
waliyoipata kupitia mada zilizowasilishwa.
Bw. Kitinga ameongeza kuwa, kupitia kikao kazi hicho Watendaji
wa Serikali mkoani Mwanza kwa kiasi kikubwa wametatuliwa
changamoto zao kiutumishi zilizokuwa zikiwakabili katika maeneo
yao ya kazi.
“Tumepata fursa za kutatua matatizo yetu kutokana na ufafanuzi
wa masuala mbalimbali ya kiutumishi uliofanyika ’’ Bw. Kitinga
amesema.
Kikao kazi hicho kimehudhuriwa na Wakuu wa Wilaya, Watendaji
wa Serikali Kuu, Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,
Wakala za Serikali, Makatibu Tawala wa Wilaya, Watendaji wa
Taasisi za Umma na Wakuu wa Sehemu/Vitengo kutoka Mkoa wa
Mwanza lengo likiwa ni kubaini changamoto zinazowakabili,
kusikiliza kero zilizopo na kuzipatia ufumbuzi ili kuboresha
mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi hao.