Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha,akizungumza na wakati akifunga mkutano mkuu wa kwanza wa wenyeviti wa walimu wakuu shule za msingi Tanzania bara uliofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Msingi kutoka TAMISEMI Dr.George Jidamva,akitoa taarifa wakati wa kufunga mkutano mkuu wa kwanza wa wenyeviti wa walimu wakuu shule za msingi Tanzania bara uliofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Umoja wa walimu (Tapsha) ambaye pia ni Mwalimu wa Makuburi Jeshini Ubongo jijini Dar es Salaam Bi.Rehema Ramole,akiongea wakati wa Mkutano Mkuu wa kwanza wa Wenyeviti wa walimu wakuu shule za msingi Tanzania bara uliofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Mwenezi wa Umoja wa walimu (Tapsha) Mwl Odas Bambaza akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha,wakati wa kufunga mkutano mkuu wa kwanza wa wenyeviti wa walimu wakuu shule za msingi Tanzania bara uliofanyika jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa kwanza wa wenyeviti wa walimu wakuu shule za msingi Tanzania bara uliofanyika jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha,akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mkutano mkuu wa kwanza wa wenyeviti wa walimu wakuu shule za msingi Tanzania bara uliofanyika jijini Dodoma.
PICHA NA ALEX SONNA-FULLSHANGWEBLOG
………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
SERIKALI imesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli kiasi cha Sh.Bilioni 943 zimetumika kwa ajili ya mpango wa elimu bila malipo.
Kauli hiyo aliitoa jijini Dodoma Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha wakati akifunga mkutano mkuu wa kwanza wa wenyeviti wa walimu wakuu shule za msingi Tanzania bara.
” Katika kipindi hicho kumekuwa na mabadiliko makubwa kwenye sekta ya elimu ambayo yamechochewa na mambo mbalimbali ikiwemo mpango wa elimu bure na ujenzi wa miundombinu.
“Kwa miaka minne sasa serikali inatekeleza mpango wa elimu bila malipo ambapo Sh.bil.24 zinatolewa kwa mwezi, na Sh.bil. 943 zimeshatumika tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani.
Alisema kuwa wanaopelekewa fedha kusimamia ni walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, hivyo isingekuwa wao kuwa wasimamizi wazuri wasingepata mafanikio makubwa.
Wakati huohuo alisema kwa kipindi hicho nchi imepiga hatua kubwa katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari ili kuwa na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia.
“Kuanzia mwaka 2016 hadi sasa zimetumika Sh.Bilioni 308 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kwa shule za sekondari na msingi, wasimamizi wakuu wa miundombinu hiyo katika ujenzi wake,”alisema.
Pia alisema kwa kipindi hicho viwango vya ufaulu vimekuwa vikipanda bila kushuka.
“Matokeo ya darasa la saba mwaka 2016 ufaulu ulikuwa wa jumla asilimia 70.2 huku mwaka 2017 ulipanda na kuwa asilimia 72.8, mwaka jana(2018) imefikia asilimia 77.72 na sifa hizi zinakuja kwenu walimu kwa kushirikiana na wazazi kw kuongeza ufaulu,”alisema.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa kidato cha nne wastani wa ufaulu kwa mwaka 2016 ilikuwa asilimia 70.4, pia mwaka 2017 ni asilimia 77.6 huku mwaka 2018 ni asilimia 78.4.
Alisema kuanzia mwaka 2016 hadi sasa serikali imeshatoa Sh.Trilioni 1.8 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu.
Ole Nasha alisema serikali inaendelea kushughulikia tatizo la upungufu wa walimu.
“Ombi la walimu wakuu kupatiwa pikipiki naomba nilibebe ni suala la kibajeti, ni kweli mngeweza kusaidia mafanikio makubwa ,”alisema.
Naibu Waziri huyo alisema serikali inajipanga kupitia sera ya elimu ili kuendana na mifumo ya ufundishaji ya karne ya 21.
Awali Mwenyekiti wa Umoja wa walimu hao(Tapsha),Rehema Ramole alisema siku mbili za mkutano huo wamepata mafunzo mbalimbali ya uongozi, haki na wajibu wao na kukabiliana na rushwa.
“Naomba walimu wakuu hao wapatiwe pikipiki ili kurahisisha usafiri kutokana na kufanya kazi kwenye mazingira magumu”alisema.