************************
Na Queen Lema Arusha
Aliyekuwa waziri wa mipango wa serikai ya mpito ya Rwanda Bw. Augustine Ngirabatware ameshindwa kuwasilisha ushahidi wa kutosha wenye uwezo wa kuaminika katika kikao cha rufaa cha mahakama ya kimataifa inayoshughulikia masalia ya makosa ya mauaji ya kimbari ili kuweza kubatilisha hukumu ya awali anayendelea kuitumikia.
Rais wa mahakama hiyo Jaji Theodor Meron amesema kuwa kupitia kifungu cha sheria namba 147 ya mwenendo wa ushuhuda Ngirabatware ambaye aliita mashahidi sita wameshindwa kutoa ushahidi wa ukweli unaounga mkono hoja mpya ya kubatilisha ushahidi wa awali uliotolewa kuwa sio wa kweli na hivyo hukumu ya awali bado inaendelea.
Mnamo Desemba 2012 mahakama ya mauaji ya kimbari ya Rwanda (ICTR)ilimtia hatiani Ngirabatware kwa kosa alilolifanya mwaka 1994 la kufanya uchochezi wa moja kwa moja wa kufanya mauaji ya kimbari na makosa ya ubakaji na kuhukumiwa miaka 35 jela na baadae Desemba 2014 mahakama ya kesi za masalia ya makosa ya mauaji ya kimbari iliondoa kosa la ubakaji na kubaki na kifungo cha miaka 30.
Aidha Julai 8 mwaka 2016 Ngirabatware aliwasilisha ombi la kupitia upya hatia yake na Juni mwaka 2017 mahakama hiyo iliridhia kusikiliza kusikiliza shauri lake upya ambapo kesi hiyo ilianza kusikilizwa september 16 hadi 27 mwaka huu.