VIJANA wa hamasa wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Mzinga, Ukonga, Dar es Salaam, wakiimba na kucheza wakati wa Kongamano la Mzinga ya Kijani baada ya kuzinduliwa juzi.
********************************
Na MWANDISHI WETU
VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kufanyia kazi
minong’ono dhidi ya wanachama wanaotarajiwa kuchukua fomu kugombea
kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, kwani ndio maoni halisi ya wananchi juu ya mgombea wanayemtaka.
Hayo yalisemwa na mgeni rasmi Gwantwa Alex ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana Taifa (UVCCM), wakati akizindua kongamano la Mzinga ya Kijani lililofanyika Kata ya Mzinga, Ukonga, Dar es Salaam, juzi.
Akizungumza mbele ya wanachama zaidi ya 300 waliohudhuria kongamano hilo
katika ukumbi wa Mkwabi baada ya kupandisha bendera katika mashina matatu
yaliyoko tawi la Mwanagati, Kinzudi na Mzinga, Gwantwa alisema ili Chama
kiweze kupata ushindi kwa asilimia 100 katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa, kuna haja viongozi kuzingatia matakwa ya wananchi kwa vile hiyo ndio njia salama ya wagombea wake kushinda.
“Nia tufike asilimia 100 ya ushindi, lakini lazima wagombea wawe wanauzika
tukikosea kuheshimu matakwa ya wananchi hatari yake ni kushindwa halafu
lawama zinabaki kwa viongozi pekee,” alisema.
Gwantwa alisema hata sababu ya CCM kushindwa katika mitaa miwili ya Mwanagati na Mzinga inayoshikiliwa na wapinzani ukiacha Magole, ilisababishwa na wananchi kutopelekewa wagombea waliowataka, ikiwamo viongozi na wanachama wake kuendekeza nongwa na ubinafsi hali iliyochangia anguko hilo.
Alisema kwa sababu hiyo ameamua Kata ya Mzinga iwe kanda maalamu kwa
dhamira ya kuhakikisha mitaa iliyopotea inakombolewa katika uchaguzi ujao, huku akiwasihi viongozi kujipanga vyema kupata wagombea sahihi watakaoungwa mkono na ndani na nje ya Chama.
Mjumbe huyo alisema anaondoka akiwa na picha ya ushindi mnono katika
uchaguzi unaokuja kutokana na kuvutiwa na mshikamano, umoja na upendo
alioshuhudia kutoka kwa viongozi wa ngazi ya kata, matawi hadi shina kuanzia
Chama na jumuia zake.
Gwantwa pia aliwataka wanachama wa CCM kujibu kwa hoja nzito vijembe vya
wapinzani na kuwasihi kujenga utamaduni wa kukisemea Chama kwa mambo
mazuri yanayofanywa kwenye utelekezaji wa Ilani.
“Kila mmoja akisemee Chama pia, viongozi jiongezeni kwa kutatua changamoto
bila kusubiri aje mwenyekiti wa kata au diwani ama kiongozi wa kitaifa… fanya
ukiona huwezi waahidi wananchi umezichukua changamoto zao unapeleka ngazi
ya juu na ukipewa majibu wapeni mrejesho wajue kinachoendelea,” alisema.
Vile vile alitaka viongozi wa Chama na watendaji wa mitaa na kata, kuwaheshimu wenyeviti wa mashina kwa vile ndiyo wenye wananchi hivyo wanajua changamoto na taarifa zote kutokana na kuishi nao mitaani na kusisitiza suala la kuwapa vitambulisho viongozi hao linapaswa kutelekezwa kwa vile ni agizo la Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mzinga, Fred Majaliwa, alimuhakikishia mgeni huyo
wamejipanga vizuri kwa ajili ya kupata ushindi wa kishindo kwa kuwa viongozi wa Chama na jumuia zake wana uhusiano mzuri.
“Mzinga ni kata mpya takwimu zinaonesha hatukufanya vizuri katika uchaguzi
uliopita wa serikali za mitaa, lakini nakuhakikishia mgeni rasmi viongozi
tumejipanga kukomboa mitaa miwili na kutetea mtaa wetu wa Magole,” alisema
Majaliwa.
Diwani wa Mzinga, Job Isack alisema kata hiyo imenufaika kufuatia vikundi 35 vya wanawake na vijana kupata mikopo ya Manispaa ya Ilala, pia kinajengwa kituo cha afya cha ghorofa moja, shule zina huduma ya maji, umeme na changamoto inayoendelea kutatuliwa ni ubovu wa barabara.
Uchaguzi wa serikali za mitaa ipatayo 4,264 nchini umepangwa kufanyika
Novemba 24, mwaka huu, ambapo utafanyika baada ya wenyeviti walioingia
madarakani mwaka 2014 kumaliza muda wa kukaa madarakani.