Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akisalimiana na Mzee wa Makazi ya Wazee Ngehe yaliyoko Wilaya Nyasa Mkoani Songea Bi. Regina Tilya wakati alipotembelea Makazi hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akisalimiana na Wazee wa Makazi ya Wazee Mkaseka yaliyoko Masaki Mtwara alipotembelea Makazi hayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akiongea na Wazee wa Makazi ya Wazee Nandanga yaliyoko nje Kidogo ya Mji wa Ndanda mkoa wa Lindi alipotembelea Makazi hayo.
Baadhi ya Wazee wa Makazi ya Wazee Mkaseka yaliyoko Wilaya ya Masaki Mtwara wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu alipotembelea Makazi hayo.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
Na Mwandishi Wetu- Lindi
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewaambia wazee waishio katika Makazi ya kutunza Wazee ya Serikali nchini kuwa lengo la Serikali ni kuboresha makazi hayo lakini akawataka wazee hao kurudi kujiunga tena na familia zao ili kuishi na faraja tofauti na sasa ambapo wanaishi katika mazingira kambi.
Dkt. Jingu ameyasema hayo mkoani Lindi wakati alipoyatembelea makazi ya kutunza wazee na wasiojiweza ya Nandanga kujionea huduma zinazotolewa kwa wazee waishio katika makazi hayo.
Dkt. Jingu pia amewakumbusha wazee hao umuhimu wa kuishi na familia zao na kuwataka kutambua kuwa jukumu la kwanza la kuhudumia mzee au mtu yeyote ni la familia na jamii yake.
Dkt. Jingu pia aliwataka wazee hao kutambua kuwa serikali na wadau wengine wanachangia tu huduma lakini akawataka wazee hao kutambua umuhimu wa kuishi na familia kwani familia ni ya msingi kabisa kwa wazee hao kuishi lakini pia kutoa ushauri wao kwa familia na jamii kutokana na wao kuishi miaka mingi.
Aidha Dkt. Jingu aliwataka wazee hao kuendelea kutoa msaada kwa jamii kwa kuwa wana maarifa mengi kutokana na kuishi kwa muda mrefu na kuonya kuwa kuendelea kwao kuishi katika makazi ya Serikali ni kupunguza mchango wao kwa jamii husika.
“Watumishi wa Serikali wanahudumia makazi haya wanajitahidi kufanya kazi hapa lakini wanakitu ambacho hawawezi kukitoa hata wafanye kazi namna gani kwani hawezi kutoa upendo unaopatikana katika familia ambao ni upendo wa baba na mtoto au upendo wa mtoto kwa baba” Aliongeza Dkt. Jingu.
Afisa Mfawidhi katika anayehudumia Makazi ya Wazee Nandanga Bw. Cleophas John alitaja changamoto wanazokabiliana nazo wazee katika Makazi hayo kuwa ni ukosefu wa umeme katika baadhi ya nyumba kituoni hapo, upungufu wa chakula, huduma ya usafiri na ukosefu wa nguo kwa wazee wasiojiweza changamoto ambazo zilijitokeza katika makazi mengine ikiwemo uchakavu wa miundobinu ya makazi.
Dkt. Jingu kwa nyakati tofauti ametembelea Makazi ya Wazee ya Mikoa ya Songea, Lindi na Mtwara kuangalia namna bora ya kuboresha hali katika makazi ya wazee ambapo ametembela Makazi ya Wazee Nandanga yaliyoko Lindi, Makaseka Mkoani Mtwara na Makazi ya Wazee Ngehe kilichopo Wilaya ya Nyasa Mkoa wa Songea.